Kipusa Viviane Miedema atawazwa Mwanasoka Bora wa Kike kwenye tuzo za BBC 2021

Kipusa Viviane Miedema atawazwa Mwanasoka Bora wa Kike kwenye tuzo za BBC 2021

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Arsenal na timu ya taifa ya Uholanzi, Viviane Miedema ametawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Kike wa tuzo za BBC 2021.

Miedema aliyeambulia nafasi ya pili nyuma ya beki wa Uingereza Lucy Bronze kwenye tuzo hizo mnamo 2020, ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Uholanzi na kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Uingereza (WSL).

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 alivunja rekodi ya ufungaji mabao kwenye michezo ya Olimpiki za Tokyo, Japan 2020 kwa kupachika wavuni mabao 10 kutokana na mechi nne.

Mshambuliaji Sam Kerr wa Chelsea na timu ya taifa ya Australia aliambulia nafasi ya pili mbele ya Mhispania Alexia Putellas wa Barcelona aliyeridhika na nambari ya tatu.

Wengine waliokuwa kwenye orodha ya mwisho ya wawaniaji watano wa tuzo ya Mwanasonasok Bora wa BBC 2021 ni beki Ashley Lawrence (Canada, Paris St-Germain) na winga Caroline Graham Hansen (Norway, Barcelona).

Kufikia sasa, Miedema amefungia Arsenal mabao 13 katika WSL msimu huu na anazidi kuweka historia katika muhula huu wa 2021-22 kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa WSL kuwahi kufunga bao dhidi ya kila kikosi walichokutana nacho.

Arsenal hawajapoteza mchuano wowote wa WSL kufikia sasa na wanaselelea kileleni mwa jedwali baada ya kushinda mechi saba na kuambulia sare mara moja kutokana na michuano minane iliyopita.

Miedema anawania pia tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu na anatarajiwa kuongoza kampeni za Uholanzi watakaokuwa wakiwania taji la Euro walilolishinda kwa mara ya mwisho mnamo 2017.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wanafunzi 2,000 Mukuru wapigwa jeki kielimu

Man-City wazamisha West Ham tena na kuendeleza ubabe wao...

T L