Michezo

Viwanja jijini Kisumu kukarabatiwa

June 1st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUMBI za mazoezi na michezo mbalimbali katika uwanja wa Jomo Kenyatta Sports jijini Kisumu sasa zitakuwa na sura mpya baada ya kufanyiwa ukarabati.

Viwanja vya soka, hoki, voliboli, mpira wa vikapu na netiboli ambavyo vimekuwa katika hali mbaya, vitakarabatiwa na Serikali ya Kaunti ya Kisumu kwa ushirikiana na Serikali Kuu.

Haya ni kwa mujibu wa Waziri wa Michezo katika Kaunti ya Kisumu, Achie Alai ambaye amesisitiza kwamba uwanja wa hoki utawekewa zulia jipya la kisasa.

Miaka miwili iliyopita, Kaunti ya Kisumu ilikarabati viwanja viwili vya mpira wa vikapu.

“Kumbi mbili za michezo mbalimbali zipo katika hali mbaya zaidi. Tumekutana na Waziri wa Michezo Amina Mohammed na kikosi chake mara mbili na wamekubali kutupiga jeki katika jitihada za kukarabati nyuga na kumbi mbalimbali katika kipindi cha miezi sita ijayo. Uwanja wa Jomo Kenyatta Sports sasa utakuwa wa viwango vya kimataifa,” akasema Alai.

Mnamo Alhamisi, Gavana Anyang Nyong’o na Alai aliandaa mkutano na Waziri Amina, Katibu wa Wizara Joe Okudo na Mratibu wa Wizara hiyo, Hassan Noor katika uwanja wa MISC Kasarani kufuatilia hatua za kukarabatiwa kwa uwanja wa Jomo Kenyatta Sports.

Kukamilika kwa shughuli za ukarabati wa uwanja wa Jomo Kenyatta kutapisha mechi za Ligi Ndogo kuandaliwa katika uwanja huo utakaokuwa na mahali pa mashabiki, wachezaji wa akiba na maafisa wa benchi za kiufundi kukalia, pamoja na vyumba vya wachezaji kubadilishia sare.

Vyumba vya mazoezi ya viungo, kumbi za burudani na watoto kuchezea, vyoo vipya na maegesho ni kati ya maeneo yatakayokuwa na sura mpya ugani humo.

Uwanja mwingine ambao umeanza kukarabatiwa katika Kaunti ya Kisumu ni ule wa Moi ulio na uwezo wa kubeba jumla ya mashabiki 20,000 walioketi.