Michezo

Vizingiti katika uhamisho wa Wanyama kutoka Spurs hadi Club Brugge

August 22nd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya tetesi kuwa Victor Wanyama anajiunga na miamba wa Uturuki Galatasaray kuzima kabisa na pia klabu za nchini Uingereza kutomakinikia kutwaa huduma zake kutoka Tottenham Hotspur, mabingwa mara 15 wa Ubelgiji, Club Brugge wanataka kumsaini.

Hata hivyo, kuna tatizo. Spurs imeambia Brugge kuwa italazimika kulipia Sh2.1 bilioni kupata huduma za nahodha huyu wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.

Ripoti nchini Uingereza zinasema kuwa Spurs iko tayari kuuza Wanyama, ambaye ameanza mechi 47 kwenye Ligi Kuu tangu anunuliwe na Mauricio Pochettino kutoka Southampton kwa Sh1.4 bilioni mwaka 2016.

Kiungo huyu mkabaji mwenye umri wa miaka 28 amekuwa akisumbuliwa na majeraha kwa misimu miwili iliyopita. Kuwasili kwa kiungo mkabaji Mfaransa Tanguy Ndombele katika kipindi kirefu cha uhamisho cha Uingereza kilichofungwa Agosti 9, kunamaanisha kuwa Spurs haihitaji huduma zake tena.

Tetesi nchini Ubelgiji zinasema kuwa Brugge imeanzisha mazungumzo na Spurs kwa nia ya kumfanya mchezaji wake kabisa. Tatizo ni kuwa Brugge inaona bei iliyotangazwa kuwa juu sana.

Gazeti la Evening Standard linaamini kuwa Brugge iko tayari kutoa Sh998.8 milioni kwa wakati huu, ingawa mazungumzo bado yanaendelea. Kuna uwezekano wa Wanyama kuchukuliwa na Brugge kwa mkopo. Hata hivyo, kuna tatizo lingine. Mshahara wake wa Sh8.1 milioni kila wiki ni kisiki kwa klabu hiyo ya Ubelgiji.

Akienda kwa mkopo, Brugge itaomba Spurs ilipie sehemu ya mshahara huu. Klabu hizi mbili zikielewana Brugge imchukue kabisa, Wanyama atalazimika kukubali kukatwa mshahara.

Klabu za Uingereza haziwezi kununua wachezaji wakati huu, lakini zinaruhusiwa kuuza kwa sababu bado mataifa mengi barani Ulaya hayajafunga vipindi vyao vya uhamisho.

Kipindi kirefu cha uhamisho nchini Ubelgiji kitafungwa Septemba 2 kwa hivyo bado kuna muda wa Brugge na Spurs kufikia mapatano.

Mpango wowote wa Brugge kuchukua Wanyama utategemea pakubwa na klabu hiyo ya Ubelgiji kuingia katika mechi za makundi za Klabu Bingwa Ulaya.

Brugge ililaza wenyeji wake LASK Linz 1-0 Agosti 20 katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kufuzu kushiriki mechi za makundi za Klabu Bingwa nchini Austria.

Itaalika kalbi hiyo nchini Ubelgiji mnamo Agosti 28. Itajihakikishia Sh1.7 bilioni ikisonga mbele.

Itaambulia Sh570.5 milioni ikibanduliwa nje na Linz.

Mikosi ya Wanyama nchini Ubelgiji

Ikiwa Wanyama atajiunga na Brugge, basi hii itakuwa mara yake ya pili nchini Ubelgiji.

Katika kipindi chake cha kwanza nchini humo, Wanyama alifanyiwa majaribio na klabu ya Beerschot AC. Alifaulu katika majaribio hayo na kuajiriwa kwa kandarasi ya miaka minne mnamo Julai 1 mwaka 2008.

Mechi yake ya kwanza ligini akivalia jezi ya Beerschot ilikuwa mwisho wa msimu 2008-2009.

Mnamo Septemba 27 mwaka 2009, Wanyama alipigwa faini ya Sh11,413 (Euro 100) na marufuku ya mechi tatu kwa kuchezea mshambuliaji mwenye uraia wa Ubelgiji na Argentina Matias Suarez wa klabu ya Anderlecht vibaya.

Aliwahi kukutana na Brugge katika Ligi Kuu ya Ubelgiji mara tatu ikiwemo mara mbili timu yake ilipolishwa kichapo cha mabao 4-1 mwaka 2010.

Katika kipindi uhamisho kirefu cha mwaka 2010, miamba wa Scotland, Celtic, walijaribu kumsaini Wanyama, lakini Beerschot ikakataa.

Miamba wa Urusi, CSKA Moscow, pia walijaribu kumsaini, lakini bila mafanikio.

Bao la kwanza la Wanyama akichezea Beerschot liliwasili Desemba 11 mwaka 2010 dhidi ya Westerlo.

Alihakikisha timu hiyo alama moja aliposawazisha 1-1 dakika ya 77 baada ya raia wa Bosnia & Herzegovina Adnan Custovic kummegea pasi.

Mikosi ya kupigwa marufuku mechi tatu ilimwandama tena Aprili mwaka 2011.

Aliadhibiwa baada ya ushahidi katika video kuonyesha alipiga kumbo mchezaji Brecht Dejaeghere wa K.V. Kortrijk.

Alichezea Beerschot mechi 54 katika mashindano yote zikiwemo 49 kwenye ligi kabla ya kujiunga na Celtic kwa Sh112.3 milioni mnamo Julai 9 mwaka 2011.

Alipata umaarufu mkubwa Celtic ikiwemo kufungua ukurasa wa magoli ikilima miamba wa Uhispania Barcelona 2-1 uwanjani Celtic Park mwaka 2012 kabla ya kununuliwa na Southampton mwaka uliofuata kwa Sh1.4 bilioni.