Vuguvugu kutoa mwaniaji ugavana

Vuguvugu kutoa mwaniaji ugavana

NA MAUREEN ONGALA

WANASIASA wanaopanga kuwania ugavana katika Kaunti ya Kilifi kupitia ODM, wanaendeleza mashauriano ya kuungana kutafuta mgombeaji mmoja atakayerithi kiti hicho cha Gavana Amason Kingi ifikapo Agosti.

Chini ya vuguvugu la Azimio la Mageuzi, wanasiasa hao wamesema lengo lao ni kutafuta mgombeaji ambaye wana hakika atafanikiwa kushinda uchaguzini na asiye na doa la kimaadili machoni pa umma.

Kundi hili linajumuisha Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi, Bw Jimmy Kahindi, Naibu Gavana Gideon Saburi na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw Dan Kazungu ambao wote ni wanachama wa ODM.

“Tunaangalia jinsi tunaweza kushirikiana ili mmoja wetu aweze kuibuka atakayepeperusha bendera hiyo. Hakuna masuala ya kupigana chenga hapa kwa vile tunaaminiana na kuheshimiana,” akasema Bw Saburi.

Bw Saburi ambaye ndiye mwanzilishi wa Azimio la Maeguzi alisema wanaangalia pia uzoefu wa mgombea na masuala ya uongozi.

Aliongeza kuwa, muungano huo unatarajia kuwajumuisha pia wanasiasa wa vyama vingine wanaotaka kuwania ugavana Kilifi ili kuona iwapo wanaweza kuunga mkono mgombeaji mmoja.

Kufikia sasa, Bw Baha Nguma anayepanga kuwania ugavana kupitia Chama cha Kadu Asili ameashiria nia ya kujiunga na mashauriano hayo.

Kwa mujibu wa Bw Saburi, hatua hiyo hata hivyo inalenga kuwatenga viongozi ambao maadili yao yanatiliwa shaka hasa kuhusiana na sakata za ufisadi.

Raslimali

“Tunataka watu wa Kilifi wapate faida katika raslimani zinazoletwa katika kaunti. Tunataka kubadili dhana ya kuwa watu wanataka uongozi ili wajinufaishe wao wenyewe. Sisi tunataka kuchukua uongozi ili watu wa Kilifi wafaidike,” akasema.

Endapo watafanikiwa kuelewana, huenda wakazuia uwezekano wa mgawanyiko chamani kuhusu mgombeaji ugavana.

Akizungumza katika eneo la Watamu, Bw Kazungu alisema mwelekeo huo utasaidia kupata kiongozi bora.

“Ukiwa kiongozi au unanuia kuwa kiongozi, huwezi kutembea peke yako bali unafaa kushirikiana na viongozi wenzako. Tuliamua pamoja na ndugu yangu ambaye ni naibu gavana tushauriane na pia tulete pamoja viongozi wengine walio na maono sawa na yetu,” akasema.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Nguma alifafanua kwamba itabidi wanachama wa ODM waamue yule ambaye wangependa awe mgombeaji wa chama hicho ili kurahisisha majadiliano na vyama vingine.

Alisema ana matumaini makubwa kuwa mwelekeo huo utazaa matunda.

“Ikiwa lengo ni kupeleka Kilifi mbele na si ubinafsi, tutaelewana na hatutakuwa na mvutano kwa sababu kile ambacho kipo tutambue kiti ni kimoja na serikali ni moja. Madhumuni ya kuja pamoja ni kuunda serikali ambayo ina uwiano. Ikiwa tumekubaliana kuhusu atakayepeperusha bendera, tutakuwa tumekubaliana serikali itaundwa vipi,” akasema.

Wanasiasa wengine ambao wanalenga kuwania ugavana katika kaunti hiyo ni Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ambaye huegemea Chama cha United Democratic Alliance (UDA), na wakili George Kithi wa Chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

You can share this post!

Hasara upepo ukizidisha dhoruba Bahari Hindi

GWIJI WA WIKI: Damaris Ketrai

T L