HabariSiasa

Vunjeni 'Tangatanga' na 'Kieleweke', Kiunjuri ashauri

June 24th, 2019 1 min read

GRACE GITAU na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Kilimo Mwangi Kiunjuri amewashauri wanasiasa wa Jubilee kuvUnjilia mbali kambi zao na kusubiri mwelekeo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhusu siasa za urithi.

Akiongea katika eneo la Mukurwei-ini mnamo Jumapili, waziri Kiunjuri pia aliwaonya wanasiasa wa kutoka Mlima Kenya dhidi ya kumhujumu Rais Kenyatta.

Bw Kiunjuri, ni mmoja wa viongozi wanaotaka kumrithi Rais Kenyatta kama kiongozi wa siasa eneo la Mlima Kenya, alikariri haja ya viongozi kutoka eneo hilo kuzungumza kwa sauti moja na kuunga mkono serikali.

“Jamii ya Wakikuyu inapasa kukumbuka kuwa wajibu wa viongozi ni kuwaleta watu wao pamoja. Wakiendelea kukorofishana, wanajamii watagawanyika,” akaonya.

Wabunge wa Jubilee wamegawanyika katika mirengo miwili; kuna wale wanaounga mkono azma ya Naibu Rais Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta mnamo 2022 wanaojulikana kama “Team Tanga Tanga” na kundi la “Kieleweke” kinachojumuisha wabunge wanaopinga ndoto ya Ruto kuingia Ikulu.

Rais Kenyatta amekuwa akitoa wito kwa wanasiasa kuweka kando siasa za urithi na kuelekeza juhudi zao katika masuala ya maendeleo.

Lakini baadhi ya wabunge wanaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu 2022, wamemkaidi Rais Kenyatta na kuendelea kumpigia debe Dkt Ruto.

Akirejelea uasi huu, Bw Kinjuri aliwaonya wabunge wa Mlima Kenyatta dhidi ya kumkaidi Rais Kenyatta akisema hatua itapelekea eneo hilo kukosa uwakilishi katika serikali ijayo.

“Hapa Mlima Kenya tuna kiongozi mmoja pekee na si mwingi ila Rais Kenyatta. Tukigawanyika tutapoteza,” akawaambia mkutano wa hadhara baaada ya kusambaza mbegu za parachichi kwa wakulima wa eneo hilo.