Habari Mseto

Vuta n'kuvute yaendelea City Hall

October 25th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MZOZO katika bunge la kaunti ya Nairobi ulionekana kuendelea kutokota Alhamisi baada ya karani wa bunge hilo Jacob Ngwele kupewa likizo ya lazima ya siku 30.

Hatua hiyo ilichukuliwa na Bodi ya Huduma za Bunge hilo la Kaunti chini ya uenyekiti wa Spika Beatrice Elachi.

Akiwa likizoni, karani huyo atachunguzwa kuhusiana na madai kuwa alivuruga shughuli za bunge hilo la Kaunti ya Nairobi.

Duru zasema kuwa inadaiwa Bw Ngwele amekuwa akilemaza shughuli za bunge hilo kwa kuwachochea wafanyakazi wachelewe kuripoti kazini.

Vilevile, inasemekana kuwa karani huyo hajakuwa akihudhuria mikutano ya bodi hiyo.

“Tumekubaliana kama bodi kumtuma Karani wetu kwa likizo ya lazima ya siku 30 kuanzia Oktoba 24, 2019. Wakati wa kipindi hicho, ameagizwa asifike katika bunge la kaunti hadi uchunguzi kuhusu mienendo yake utakapokamilika,” akasema Elachi.

Apata agizo la mahakama

Hatua hii inajiri siku mbili baada ya Bw Ngwele kupata agizo la mahakama kuzuia bodi mpya iliyozinduliwa na Spika kuhudumu.

Pia agizo hilo lilisimamishwa kwa muda kuondolewa kwa kiongozi wa wengi Abdi Guyo na kiongozi wa wachache Elias Otieno kama wanachama wa bodi hiyo.

Wawili hao walipokonywa nafasi zao na vyama vyao.

Chama cha Jubilee kiliteua diwani wa wadi ya Maringo Hamza Mark Ndung’u mahala pa Guyo huku diwani wa Nairobi West Maurice Gari akipewa nafasi ya Bw Otieno ambaye ni diwani wa Kileleshwa.

Wengine walioondolewa kutoka bodi hiyo ni pamoja na Ada Onyango ambaye ni naibu karani wa bunge la Kaunti ya Nairobi, Philomena Nzuki ambaye ni Mhasibu Mkuu, Nancy Mutai ambaye ni afisa wa wafanyakazi na Garvin Castro ambaye ni msaidizi wa karani.

Agizo hilo lililotolewa na Jaji wa Mahakama ya Ajira na Masuala ya Leba Onesmus Makau linasitisha utekelezaji wa mabadiliko katika bodi kama ilivyochapishwa na Spika Elachi katika gazeti rasmi la serikali hadi kesi hiyo itakapoanza kusikizwa mnamo Novemba 11 na uamuzi kutolewa.

Licha ya kusimamishwa kwake, Bw Ngwele amesisitiza ataendelea kutekeleza majukumu yake kama karani, akisema hakuna mkutano wa bodi ulioitishwa kumsimamisha kazi kwa sababu shughuli zake zilizokuwa zimesimamishwa na agizo la mahakama.

“Kwa hivyo, uamuzi wa Spika hauna maana, na nitaukaidi. Vilevile, nitamshtaki kwa kudharau mahakama,” akasema Ngwele.

Karani huyo ambaye pia ndiye Katibu wa Bodi ya Huduma za Bunge la Kaunti ya Nairobi alisema bodi hiyo haiwezi kufanya mkutano bila Katiba na hivyo akataja uamuzi wa Spika Elachi kama batili.