Habari

Vuta n'kuvute yaendelea UoN

January 22nd, 2020 2 min read

FAITH NYAMAI na OUMA WANZALA

NAIBU Chansela wa Chuo Kikuu Cha Nairobi (UoN) Stephen Kiama ambaye anaomgoza asasi hiyo muhimu kufuatia agizo la mahakama ya masuala  ya leba, sasa anasema amenyimwa funguo za kuingia ofisini mwake.

Katika memo iliyotumwa kwa wanafunzi wa chuo hicho pamoja na wafanyakazi, Prof Kiama – ambaye uteuzi wake ulisitishwa na Waziri wa Elimu Prof George Magoha – amesema Jumatano analazimika kutumia ofisi mbadala.

Amedai kwamba Prof Isaac Mbeche ambaye Prof Magoha alimteua kaimu naibu chansela, amekataa kumkabidhi funguo za ofisi hiyo iliyoko katika Orofa ya 3 katika jengo maarufu la UoN Towers.

“Ikiwa ni njia ya kulinda hadhi ya chuo kikuu ili kisije kikaharibiwa, naibu chansela atatumia ofisi iliyoko katika orofa ya 19 ya jengo la UoN Towers,” amesema Prof Kiama.

Ameongeza kwamba hatua yake ni ya kudumisha utiifu katika sheria na utaratibu wa chuo hicho chenye hadhi kubwa kote nchini na kimataifa.

Jumanne Prof Kiama alitangaza kumtuma Prof Mbeche kwa likizo ya kila mwaka ambayo alisema ilianza Januari 6 na ikiwa ni kufuatia ombi alilotuma mwenyewe.

Prof Mbeche ni makamu wa naibu chansela anayeshughulikia masuala ya fedha, upangaji na maendeleo.

Prof Kiama alimteua Prof Madara Ogot ambaye ni makamu wa naibu chansela anayeshughulikia masuala ya utafiti kuchukua majukumu ya Prof Mbeche wakati akiwa likizoni.

Ni hatua iliyomghadhabisha Prof Mbeche ambaye aliipuuzilia mbali.

Pia akitangaza uteuzi huo, Prof Kiama alijaza nafasi moja zaidi.

“Vilevile Prof Julius Ogeng’o, makamu wa naibu chansela anayeshughulikia masuala ya masomo, ameteuliwa katika nafasi ya ukaimu awe makamu wa naibu chansela anayeshughulikia masilahi ya wanafunzi hadi nafasi hiyo itakapojazwa,” akasema Prof Kiama.

Kwa upande wake Prof Mbeche alisema japo alikuwa likizoni, alilazimika kurejea kazini baada ya kuitwa na waziri Magoha. Ingawa hivyo, alisema alikaa mbali na ofisi hiyo ikiwa sehemu ya kutii agizo la mahakama.

“Tunasubiri uamuzi wa serikali baada ya agizo la mahakama lililotolewa Jumatatu,” akasema Prof Mbeche.

Mapema Jumatano wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho wameandaa mikutano tofauti kujadili hali na mustakabali wa UoN.

Baadhi ya wafanyakazi hao na wanafunzi wanavutia upande wa Prof Kiama huku wengine wakiunga Prof Mbeche.

Hali ya vuta n’kuvute inayoshuhudiwa chuoni humo sasa inasababisha wasiwasi kuhusu heshima ya asasi hiyo.

Katibu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Kiakademia wa Vyuo Vikuu (Uasu), katika UoN, Dkt George Omondi, ametaka mgogoro huo usuluhishwe mara moja.

“Huwa tunafanya ujima na ushirikiano na asasi za kimataifa na wakiona tukizozana wenyewe kwa wenyewe, hatutafaulu katika masuala tunayotaka kufanikisha,” amesema Dkt Omondi.