Habari Mseto

Vyama 7 vya matatu vyapigwa marufuku na NTSA

October 31st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) imefutilia mbali usajili wa vyama saba vya magari ya uchukuzi wa umma.

Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumanne, NTSA ilisema kuwa Sacco hizo zilisimamishwa Septemba 13, 2018, bila kuelezea sababu.

Lakini huenda ni kutokana na malalamishi ya uendeshaji mbaya wa magari au kusababisha ajali.

Sacco hizo ni Molo Shuttle ambayo hutumia barabara ya Nairobi, Nakuru, Olenguruone na Kisii, Nairobi Kiruline Sacco inayotumia barabara ya Nairobi, Murang’a, Othaya, Nyeri na Nyahururu, Gakanago Sacco ambayo hutumia barabara Nyeri, Gataragwa na Ngobit, New Lowland Sacco ambayo hutumia barabara ya Nakuru, Maraigat na Kabarnet, Hannover Commercial Enterprise inayotumia Kikuyu, Waiyaki Way, Westlands, Tom Mboya, Thika Road, Kasarani na Mwiki.

Sacco zingine zilizofutiliwa mbali ni Newlot Sacco ambayo hutumia barabara ya Nairobi, Machakos, Makueni, Kitui, Mutomo, Kibwezi, Ikutha, Voi na Mombasa.

Pia, magari yanayohudumu chini ya Peja Travellers katika mitaa ya Jericho, Maringo, Jogoo Road na Temple Road yalisimamishwa.

Kumekuwa na ongezeko la visa vya ajali nchini ambazo zimesababisha vifo vya mamia ya abiria na kujeruhi wengine.