VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya Upili ya Kambiti, Meru (CHAKIKA)

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya Upili ya Kambiti, Meru (CHAKIKA)

NA CHRIS ADUNGO

KATIKA jitihada za kuwapa wanafunzi majukwaa mwafaka zaidi ya kujiimarisha kimasomo na kukuza talanta katika sanaa mbalimbali, shule ya upili ya Kambiti iliyoko Kaunti ya Meru ilianzisha Chama cha Kiswahili (CHAKIKA) mnamo 2018.

Mbali na kuweka wazi umuhimu wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi kwa kupiga jeki juhudi za Idara ya Kiswahili inayosimamiwa na Bw Kinoti, madhumuni mengine ya CHAKIKA ni kustawisha makuzi ya lugha kwa kuzidisha maarifa ya utafiti katika fani zinazofungamana na Kiswahili.

Bi Stella Nkonge ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Kambiti, naye amejitolea sabili kuunga mkono mikakati ya CHAKIKA kwa kuhakikisha kuwa kinafadhiliwa ipasavyo kila kinapoandaa makongamano ya Kiswahili na kushirikisha wanachama katika mradi wa usomaji wa gazeti la Taifa Leo shuleni.

Zaidi ya kuhamasisha jamii kuhusu masuala muhimu kupitia michezo ya kuigiza, wanachama wa CHAKIKA wamefaulu pia kudhihirisha weledi wao katika utunzi wa mashairi ambayo huchapishwa katika gazeti la Taifa Leo.

Vipaji vya ulumbi, utambaji wa hadithi na uimbaji navyo vimeimarika sana miongoni mwa wanafunzi wa Kambiti ambao sasa wanatumia CHAKIKA kama chombo madhubuti cha kuwaamshia hamu ya kuwa wanahabari, walimu na wahariri katika siku za usoni.

Kubwa zaidi katika maazimio ya CHAKIKA ni kuimarisha kitengo cha maigizo kwa nia ya kuigiza vitabu vyote teule vinavyotahiniwa katika shule za sekondari nchini.

Changamoto kuu kwa chama ni msimbo wa Sheng ambao umezoeleka sana miongoni mwa wanafunzi wengi.

Hata hivyo, chama kimejitolea kushirikiana na vyama vingine shuleni ili kutoa fursa kwa wanafunzi kuhamasishana kuhusu mafao ya Kiswahili na nafasi ya lugha hii katika soko la ajira. Wanachama hukutana pia mara kwa mara kwa nia ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu uandishi wa insha na kuzamia baadhi ya mada zinazowatatiza madarasani.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Angie Magio

NGUVU ZA HOJA: Kiswahili ni mhimili mkuu wa kuhifadhi...

T L