VYAMA: Chama cha Uanahabari katika Shule ya Upili ya St Martha’s Mwitoti, Mumias, Kakamega

VYAMA: Chama cha Uanahabari katika Shule ya Upili ya St Martha’s Mwitoti, Mumias, Kakamega

NA CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Uanahabari katika shule ya upili ya St Martha’s Mwitoti ni jukwaa linalotumiwa na wanafunzi wa shule hii iliyoko Kaunti ya Kakamega kuchapukia masomo ya lugha.

Mbali na kutambua na kulea vipaji vya wanafunzi katika sanaa mbalimbali, madhumuni mengine ya chama hiki ni kuchochea maadili miongoni mwa wanafunzi na kuwaamshia hamu ya kujitosa katika ulingo wa uanahabari baada ya kukamilisha KCSE.

Chama kwa sasa kinajivunia zaidi ya wanachama mia moja wakiongozwa na Dalton Machio (Mwenyekiti), Jessica Sakwa (Mhariri), Betty Auma (Katibu) na Khalif Wambani (Mratibu).

Mlezi wa chama ni Bw Simon Musiku anayefundisha Kiingereza na Fasihi shuleni Mwitoti.

“Chama kimevusha wanafunzi katika masuala ya kiakademia na kuboresha matokeo ya mitihani katika masomo ya Kiswahili na Kiingereza. Isitoshe, viwango vya wanafunzi katika michezo ya kuigiza, utambaji wa hadithi, uandishi wa insha na utunzi wa mashairi pia vimeimarika,” anasema mwalimu wa Kiswahili, Bw Boniface Ambunya.

Wanachama hukutana kila Jumanne kuanzia saa kumi hadi saa kumi na moja na robo jioni kujadili maendeleo ya chama na kuweka mikakati ya jinsi ya kukusanya habari za matukio mbalimbali kabla ya kuzihariri na kuziwasilisha gwarideni.

Kubwa zaidi katika mipango ya chama kwa sasa ni kukutanisha wanafunzi na baadhi ya wanahabari na waandishi maarufu wa Kiswahili humu nchini kwa nia ya kuwaelekeza na kuwachochea zaidi kitaaluma.

Mbali na kusoma habari gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa, wanachama wamezamia pia uchapishaji wa jarida la Kiswahili linalopania kuwapa wanafunzi fursa ya kuchangia makala ya kitaaluma na kazi bunilizi.

Manufaa ya chama yanazidi kuonekana kwani wanafunzi wengi kwa sasa shuleni Mwitoti wanatia fora katika somo la Kiswahili huku wanachama wakishiriki Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti la Taifa Leo.

  • Tags

You can share this post!

RIWAYA: Sifa za Neema na jinsi anavyoendeleza ploti katika...

Kibarua kigumu cha Okutoyi robo-fainali ya tenisi ya...

T L