Habari MsetoSiasa

Vyama vidogo vyadai kupuuzwa katika BBI

February 6th, 2020 2 min read

NA BRENDA AWUOR

WAWAKILISHI wa vyama kadhaa vya kisiasa, wamelalamika kwamba ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) haikujumuishi maoni ya vyama vyote vya kisiasa.

Baadhi ya wawakilishi wa vyama walisema, jinsi ilivyo sasa, ripoti hiyo ina maoni ya vyama vilivyohusishwa katika handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga pekee.

Walikuwa wanazungumza wakati wa mkutano baina ya wawakilishi wa vyama 68 na kamati ya vyama vya kisiasa ulioandaliwa Kisumu jana, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuhusu ripoti ya BBI waliposema ni sharti ripoti ifanyiwe marekebisho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kushirikisha Vyama vya Kisiasa, Bw Irungu Nyakera, aliambia wanahabari kuwa wito utatolewa kwa jopo la BBI kuzingatia malalamisho ya vyama hivyo kwenye ripoti ya mwisho itakayotolewa kabla ya kura ya maoni kufanywa endapo itahitajika.

“Tunaomba wanajopo wa ripoti ya maridhiano kujumuisha malalamishi haya kabla ya kura ya maoni,” akasema.

Wawakilishi kutoka vyama vya Ford Kenya, Uzalendo, Independent, Ford Asili, miongoni mwa vingine wametoa sababu kadhaa ya marekebisho.

Bw Julius Wambua, mwakilishi wa chama cha Independent, alisema kuwa ripoti ya maridhiano ni suala la kitaifa kwa hivyo ni lazima ihusishe maoni ya raia na haipaswi kuhusisha maoni kutoka kwa viongozi wa vyama viwili tu.

Kwa kurejelea sehemu ya ripoti inayozungumzia suala la maridhiano, alisema kuwa, ripoti imehusisha maoni ya watu wachache.

Maoni yake yaliungwa mkono na wawakilishi wengine waliosisitiza kwamba watu waliotoa maoni yaliyojumuishwa kwenye ripoti ni kutoka Chama cha ODM na Jubilee pekee, na maoni ya vyama vingine yakaachwa nje.

Bi Jane Njiru, mwakilishi wa chama cha Ford Asili, alipendekeza kuwa vyama vyote ambavyo vimesajiliwa vijumuishwe katika ripoti ya maridhiano, bila kujali kama chama kinaunga mkono BBI au la.

Bi Njiru alieleza kuwa si sawa vyama viwili kunyakua mpango wa serikali na kutumia rasilimali za kitaifa vibaya kwa madai ya kuhamasisha wananchi, huku vyama vingine vikiachwa kutazama kutoka pembeni.

“Vyama vyote viwekwe ndani ya mpango huu kisha rasilimali pamoja na fedha kugawanywa kwa kila chama wakati wa hamasisho,” alieleza.

Baadhi ya wawakilishi walilalamika kwamba jana ndipo walipokea ripoti ya maridhiano kwa mara ya kwanza, ishara kwamba mwananchi wa kawaida hajaiona kufikia sasa ilhali magavana kadhaa wanatangaza kwamba wananchi wameikubali.

Mwakilishi wa Ford Kenya, Bw Joe Ruhu pamoja na Bw Saja Philipo wa Chama cha Uzalendo walitetea ripoti ya BBI lakini wakasema mapendekezo na malalamishi kutoka kwa vyama vingine pia yashughulikiwe.