Vyama vipya vinaundwa kwa misingi ya ukabila – Msajili

Vyama vipya vinaundwa kwa misingi ya ukabila – Msajili

NA MWANDISHI WETU

MSAJILI wa Vyama vya Kisiasa, Bi Ann Nderitu, ameeleza hofu kuhusu ongezeko la vyama vya kisiasa vinavyoegemea ukabila nchini uchaguzi mkuu unapokaribia.

Alisema afisi yake imeanza kupanga kuhusu namna ya kuimarisha na kupanua uwezo wa vyama vya kisiasa vilivyopo kuzima hali hiyo.

“Kuanzia sasa, usajili wa vyama vya kisiasa utajikita kuhusu falsafa na manifesto zake. Vyama lazima viendeleze umoja miongoni mwa Wakenya. Vyama hivyo na wanasiasa vinatarajiwa kuhubiri amani na umoja badala ya kuzua migawanyiko baina ya jamii nchini. Ni vyama vilivyo na mitazamo ya kitaifa pekee ambavyo vitasajiliwa,” akasema Bi Nderitu.

Alitoa kauli hiyo jana, alipomtembelea Gavana Francis Kimemia wa Nyandarua afisini mwake.Kwa muda sasa, vyama vipya vimekuwa vikisajiliwa baadhi vikihusishwa na vigogo wakuu wa kisiasa.

Naibu Rais William Ruto tayari ameonyesha wazi kuunga mkono chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho nembo yake ni wilbaro.

Katika eneo la Pwani, viongozi mbalimbali wa mirengo yote wamekuwa wakitoa wito kuundwe chama cha kutetea maslahi ya jamii za ukanda.Vile vile, katika eneo la magharibi, vyama vya Ford Kenya na Amani National Congress vimezidisha juhudi za kudhibiti siasa za eneo hilo.

Gavana Kimemia jana alitangaza uwezekano wa kubuniwa chama kingine cha kisiasa karibuni. kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, au muungano wa vyama vinavyoegemea mrengo wa Jubilee.

“Wakati umefika kwa Chama cha Jubilee (JP) kuwachukulia hatua wanasiasa waasi chamani. Tunapaswa kukilainisha na kukipa nguvu chama chetu ili kuendelea mbele. Hakuna jambo lolote linalotuzuia kuungana na vyama vingine kama ODM,”akasema.

You can share this post!

Changamoto tele zinazomsubiri Biden kukabili

ODM wajuta kuingia katika handisheki bila utaratibu