Makala

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Ideal Kitengela ni nyota ya jaha

March 27th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHULE ya Msingi ya Ideal katika eneo la Kitengela, Kaunti ya Kiambu, ni miongoni mwa shule nyingi kutoka humu nchini ambazo kwa sasa zinatambua umuhimu wa mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Kupitia mradi huu, NMG inatumia gazeti lake la Taifa Leo kuimarisha viwango vya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili na masomo mengine katika shule za msingi na upili.

Bw Symon Gor Okello ambaye ni Mwalimu Mkuu na pia mwalimu wa Kiswahili katika shule hii, anakiri kwamba matokeo bora yaliyojivuniwa na wanafunzi wake katika mitihani kwa sasa ni zao la NiE, mradi ambao kwa mtazamo wake unazidi kubadilisha pakubwa sura ya usomaji na ufundishaji wa Kiswahili shuleni humu.

Kulingana na Bw Okello, wengi wa wanafunzi wake wanaothamini na kuchangamkia usomaji wa Taifa Leo na kushiriki Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili hudumisha umahiri wao katika lugha kwa kukwangura alama za juu zaidi katika mitihani ya Kiswahili.

Walimu na wanafunzi shuleni Ideal pia wanasifia majaribio ya mitihani ambayo huchapishwa katika gazeti hili la Taifa Leo kati ya miezi Februari na Novemba kuwa mhimili mkubwa unaozidi kuchangia matokeo bora ya wanafunzi wao katika mitihani ya kitaifa ya KCPE.

Majaribio

Shule hii ni miongoni mwa zile ambazo zimekuwa zikijinunulia nakala nyingi za magazeti ya Taifa Leo kupitia mradi wa NiE.

Bw Elijah Chewa Gichuki ambaye pia ni mwalimu wa Kiswahili shuleni Ideal, anasema kuwa majaribio hayo ya mitihani ni daraja halisi la mafanikio kwa wengi wa wanafunzi wake ambao wamechochewa kutia fora katika Kiswahili huku wakihimizwa kuyathamini masomo mengine kwa kiwango sawa.

Kwa pamoja na Bw Okello, mwalimu huyu anazisihi shule nyinginezo za humu nchini kuiga mfano wao ili kuimarisha viwango vya maandalizi ya wanafunzi wakati wanapojizatiti kuikabili mitihani ya kitaifa ya KCPE 2019.

Kauli hii inaungwa mkono na walimu wengine ambao kwa pamoja, wamepania kuhakikisha kwamba gurudumu la Kiswahili halikwami kabisa katika Shule ya Msingi ya Ideal, Kitengela.

Bw Okello anahisi kwamba tayari matunda ya uwapo wa Chama cha Kiswahili shuleni humo yameanza kuvunwa hasa ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha jinsi wanafunzi wanavyolichapukia somo la Kiswahili pamoja na jinsi wanavyotumia lugha hiyo kwa ufasaha zaidi katika mawasiliano.