VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Lelwak

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Lelwak

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Lelwak (CHAKILE) kiliasisiwa mwaka huu na walimu wapenzi wa Kiswahili katika shule hiyo iliyoko Kapsabet, Kaunti ya Nandi.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa CHAKILE ni kuimarisha na kuweka wazi umuhimu wa lugha ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Chini ya ulezi wa Bw Richard Ondoli Amunga, CHAKILE kwa sasa kiko chini ya uongozi wa Walter Aunga (Mwenyekiti). Vinara wengine wa chama hiki ni Steven Mwololo (Naibu Mwenyekiti), Leon Kiprop (Mhariri), Claudius Kipchirchir (Mhazini) na Ian Kipkurui (Afisa wa Uhusiano Mwema).

Madhumuni mengine ya CHAKILE ni kuboresha matokeo ya somo la Kiswahili katika KCSE, kubadilisha mtazamo hasi kwa Kiswahili, kuleta pamoja watetezi wa Kiswahili, kukuza talanta za wanafunzi katika kazi za kubuni, kustawisha matumizi ya Kiswahili Sanifu shuleni, kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kushirikiana na vyama vingine ili kuimarisha juhudi za makuzi ya Kiswahili.

Chama kwa sasa kina mikakati ya kushiriki makongamano mbalimbali ya Kiswahili kwa malengo ya kuwakutanisha wanafunzi na walimu, wanahabari na waandishi maarufu wa Kiswahili ambao watawaamshia hamu ya kukichapukia Kiswahili.

Aidha, kimetenga vipindi maalumu kila siku ya Jumatano ili kupitia gazeti la Taifa Leo hasa kijarida cha Lugha na Elimu kwa madhumuni ya kujifunza mengi kuhusu taaluma ya Kiswahili.

Katika juhudi za kufanikisha baadhi ya malengo yake, chama kimewapa wanafunzi jukwaa la kukuza vipawa vyao katika ulingo wa uanahabari. Wanachama hutafiti kuhusu baadhi ya matukio na masuala ibuka na kusoma habari hizo gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Chama pia kimezamia uchapishaji wa jarida la ‘Lelwak Times’ ambalo hutoa fursa kwa wanachama kuchangia makala ya kitaaluma na kazi bunilizi mara moja kwa mwaka.

CHAKILE pia huandaa kongamano la Kiswahili kila muhula ili kuwapana wanafunzi nafasi ya kujadili masuala mbalimbali katika somo la Kiswahili. Walimu wa Idara ya Kiswahili wakiwemo Amunga, Rosemary Jepkurgat, Aaron Lang’at, Nehemiah Kirui na Edwin Magut wanazidi kushirikiana na usimamizi wa shule kuhakikisha kuwa kuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili na nakala za magazeti ya Taifa Leo maktabani.

Wanachama wa CHAKILE hukutana mara kwa mara kujadili masuala mbalimbali kuhusu uandishi wa insha, sarufi na matumizi ya lugha, fasihi simulizi, ushairi na kuchambua vitabu vya fasihi andishi.

Chama pia kina huandaa vikao maalumu mara mbili kila muhula kwa lengo la kushirikisha wanachama katika mashindano yanayolenga kubaini upekee wa vipaji vyao katika kughani mashairi, kutamba hadithi, kutunga mashairi na kuigiza.

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Upili ya Lelwak, Kapsabet, Kaunti ya Nandi. Picha/Chris Adungo

Mlezi wa CHAKILE hutumia fursa hiyo kutuza washindi wa vitengo mbalimbali na kutoa nasaha za kuwatia wanachama motisha kuhusu safari ya usomi kwa jumla.

Kufikia sasa, manufaa ya chama hiki yameonekana kwani wanachama wengi wameendelea kufaulu vyema katika somo la Kiswahili na kuwapiku wenzao wanaodunisha Kiswahili na kuchapukia masomo mengine.

Licha ya kwamba hakijakomaa vilivyo, chama kimefaulu kufanya mengi shuleni chini ya kipindi kifupi ikiwa ni pamoja na kuandaa makongamano ya ndani kwa ndani, kuingia mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) na kuwapa wanafunzi fursa ya kuendesha midahalo wazi ili kuangazia masuala mbalimbali yanayofungamana na maendeleo ya jamii.

Uwapo wa chama hiki shuleni umeamsha ari ya mapenzi ya Kiswahili miongoni mwa wanachama ambao kwa sasa ni wazalendo na mabalozi wa Kiswahili na wasomaji wakuu wa magazeti ya Taifa Leo.

Changamoto zinazokabili CHAKILE ni pamoja na baadhi ya wanafunzi kutokionea fahari Kiswahili na ukosefu wa fedha za kuendesha baadhi ya shughuli ili kufanikisha maazimio mbalimbali ya wanachama.

Aidha, baadhi ya wanafunzi wana kasumba kuwa Kiswahili ni lugha duni na hakina umuhimu hivyo kupendelea zaidi masomo mengine kama vile Hisabati, Kemia na Fizikia. Wanafunzi wengine huchukulia Kiswahili kuwa somo rahisi lisilohitaji kutengewa muda zaidi kwa minajili ya mazoezi na marudio.

You can share this post!

‘Corona’ ya punda yalipuka na kuzua hofu kubwa...

GWIJI WA WIKI: Dennis Mwima