Makala

VYAMA VYA KISWAHILI: Jivunio la lugha ya Kiswahili Shuleni Mukaa Boys, Kaunti ya Makueni

June 5th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHAKIMU ni chama kinachodhamiria kuchangia matumizi bora ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys iliyoko viungani mwa mji wa Salama, Kaunti ya Makueni.

Chama hiki kiko chini ya Idara ya Lugha shuleni Mukaa Boys. Idara hii inashughulikia Kiswahili na Kiingereza na inaongozwa na Bi Hilder.

Mwalimu Mkuu, Bw Francis Mutua huhakikisha kuwa wanafunzi wanapata nakala 10 za gazeti la Taifa Leo kila siku.

Kwa mujibu wa Bw Deon Musau Muia, wanafunzi wake wanadumisha umahiri wao katika lugha baada ya kuyasoma magazeti hayo na kushiriki katika Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili kila mwezi.

Isitoshe, mashairi katika kurasa za gazeti la kila Jumamosi, Jumapili na Jumatatu huwapa wanafunzi burudani na mshawasha wa kuwa watunzi wa siku za usoni. Aidha, mashairi hayo huwanasihi sana wanafunzi.

Kwa mfano, shairi katika gazeti la Jumatatu, Juni 3, 2019, lenye mada “Mwanangu”, liliwakosha wanafunzi wengi sana shuleni Mukaa Boys ambao kwa mujibu wa Bw Deon, walipata mwamko mpya wa kuyachapukia masomo ili waiokoe jamii yao.

Shairi hilo lilitungwa na Fadhili Farjala ‘Samaki wa Jangwani’ kutoka Chuo Kikuu cha KeMU.

Wanachama hukutana kila siku ya Jumatano kuanzia saa kumi na dakika arubaini ili kuyaangazia masuala mbalimbali ya Kiswahili. Kufikia sasa, wanachama wote ni 306.

Chama hiki kina vitengo mbalimbali vinavyowasaidia wanachama kubobea katika kila sehemu ya Kiswahili.

Vitengo hivyo ni pamoja na: Kitengo cha Ushairi, Kitengo cha Sanaa na Uigizaji, Kitengo cha Sarufi, Kitengo cha Utangazaji na Kitengo cha Tafsiri na Ukalimani.

Wanachama wengi huishia kutambua talanta zao fiche kutokana na uwepo wa vitengo hivi.

CHAKIMU kipo chini ya uongozi wa Bw Deon ambaye kwa sasa ni Mlezi wa Chama.

Chama pia kina wawakilishi kutoka kila kidato wakiongozwa na Lucas Mambo (Mwenyekiti), Abaraham Kisua (Mhazini), Collins Kyengo (Mwakilishi wa Kidato cha Kwanza), Michael Muoki (Katibu), Peter Njoroge (Mwakilishi wa Kidato cha Pili), Kilei Joseph (Msimamizi wa Kitengo cha Sarufi) na Yasir Abdi (Msimamizi Kitengo cha Tafsiri).

Bw Deon anahisi kwamba matunda matamu ya uwapo wa CHAKIMU yameanza kushuhudiwa tayari kwa sababu asilimia kubwa ya wanafunzi kwa sasa hutumia Kiswahili kwa ufasaha na mantiki.