Habari Mseto

Vyama vya siasa katika mbio za kutii masharti

October 6th, 2020 2 min read

Na KENNEDY KIMANTHI

VYAMA vya kisiasa nchini viko mbioni kuhakikisha kuwa vimetimiza kanuni zote zilizo kwenye Katiba ili kutozuiwa kuwasimamisha wawaniaji kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Jambo linaloonekana kuwa kiazi moto kwa vyama vingi ni hitaji kwamba lazima viwe na idadi fulani ya wanachama kutoka maeneo yote nchini, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya 2011.

Kanuni hizo zimevifanya vyama vingi kuanza kuwasajili wanachama katika sehemu mbalimbali nchini, kwenye hatua inayoonekana kama matayarisho ya mapema ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Vyama, vilevile vinahitajika kuwa na makao makuu yenye anwani maalum na angaa wanachama 1,000 katika nusu ya kaunti zote 47.

Kulingana na stakabadhi kutoka kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, zaidi ya vyama vipya 400 vimetuma maombi ya usajili.

Kufikia Jumatatu iliyopita, vyama 83 vya kisiasa vilikuwa vishasajiliwa huku vingine saba vikingoja kusajiliwa.

Licha ya ugumu uliopo kwenye harakati za kutimiza masharti hayo, baadhi ya vyama pia vinalenga kupata mgao wa pesa zinazotolewa kwa vyama vya kisiasa na serikali.

Vyama vikubwa pekee ndivyo vimekuwa vikipata fedha hizo, huku viwango vinavyopewa vikilingana na idadi ya kura vilivyopata kwenye chaguzi zilizopita.

Mgao pia huwa unalingana na kiwango cha uwakilishi wa chama husika kwenye Bunge la Kitaifa.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, vyama vinapaswa kupewa asilimia 0.3 ya bajeti ya kitaifa.

Hapo Jumatatu, Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa ilimaliza mchakato wa kuwapa mafunzo maafisa wa vyama vipya vya kisiasa vilivyosajiliwa.

Vyama hivyo ni Grand Dream Development (GDC), United Green Movement (UGC) na Civic Renewal Party (CRP) ambacho kinahusishwa na Gavana Mwangi wa Iria wa Kaunti ya Murang’a.

Taratibu

Mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha vina taasisi thabiti na taratibu zifaazo kwenye usimamizi wake.

Vyama kama CRP vinaelezwa kufanya kila juhudi kuimarisha mwonekano katika sehemu mbalimbali nchini.

Taifa Leo imebaini chama hicho kimeanza mipango kabambe ya kuwasajili wanachama kote nchini, kwenye hatua inayoonyesha huenda kikawa na usemi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Chama hicho kina makao yake makuu eneo la Lavington, jijini Nairobi.

Makao hayo ndiko mikakati yake yote itaendeshwa kumsaidia Bw Wa Iria kujipigia debe, kwenye azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2022.

Chama cha Ford-Kenya pia kimeanza usajili wa wanachama katika kaunti za ukanda wa Mlima Kenya.

Chama hicho pia kinalenga kujiimarisha kisiasa ielekeapo 2022, kwa kuwasajili watu wengi kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo.

Akizungumza Jumatatu kwenye kikao cha wajumbe mjini Meru, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Eseli Simiyu, alisema kuwa mchakato huo unalenga kuwashinikiza watu wengi kujiunga nacho kabla ya kuandaa kongamano la kimataifa la wajumbe, ambapo kiongozi mpya atachaguliwa.

“Hatujawa tukiwasimamisha wawaniaji katika eneo hili licha ya Meru kuwa mojawapo ya ngome kuu za chama hiki. Tutakuwa tukifanya mikutano ya mara kwa mara na wanchama wetu katika kaunti mbalimbali. Lengo letu ni kurejesha umiliki wa chama hiki kwa wananchi wenyewe,” akasema.