Habari Mseto

Vyama vya ushirika Thika vichunguzwe, asema afisa

February 4th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

AFISA mmoja kutoka Thika anaitaka serikali kuchunguza kwa makini vyama vya ushirika vinavyochipuka nchini.

Mwenyekiti wa Azima Sacco ya Thika, Bw Peter Njuki, alisema kwa muda wa miezi michache iliyopita vyama vichache vimefuja pesa za wateja wao jambo ambalo limeleta shida kwa familia nyingi.

Alitaka vyama vya ushirika viwe na uwajibikaji kwa wateja wao ili nao wawe na moyo wa kuwekeza fedha zao huko.

Alisema maafisa wakuu waliochaguliwa katika vyama vya ushirika wawe na maadili mema ili wafanikishe malengo ya kuwatumikia wateja wao vyema.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati walipozuru kituo cha watoto yatima cha Revelation Centre eneo la Muguga, Thika Mashariki.

Kwa muda wa miezi michache iliyopita chama hicho cha Azima kimekuwa kikisaidia  kituo hicho kwa kuwajengea mabweni na vyoo vya kisasa kituo hicho huku pia wakiwapa vyakula .

Mwishoni mwa wiki waliweza kuzuru kituo hicho na kutoa misaada ya nguo, viatu na mahitaji muhimu ya kila siku.

Chama hicho kinajitolea kusaidia jamii katika mashinani hasa wasiojiweza.

Alisema bali na kuchunga fedha za wananchi vyama vya ushirika vinastahili kufanya juhudi na kuwafikia wasiojiweza kama mayatima na wazee.

Alisema kwa siku za hivi karibuni chama hicho cha Azima kimesaidia kituo kwa miradi zilizogharimu takribani Sh 500,000.

Kituo hicho kilichonzishwa mwaka wa 2007, kina watoto wapatao 100 kati ya miaka miwili hadi 15.

Mwanzilishi wa kituo hicho ambaye ni msimamizi, Bi Agnes Njoki Mungai, alipongeza shirika la Azima kwa kuwaletea maendeleo kadha katika kituo hicho.

“Ninashukuru Azima Sacco kwa kazi nzuri waliotufanyia kwa kutujengea bweni na vyoo vya watoto hawa yatima. Tutazidi kushirikiana nao kila mara ili tuzidi kunufaika na mazuri kutoka kwao,” alisema Bi Mungai.

Diwani wa Ngoliba Bw Joachim Mwangi alizilaumu vyama vya ushirika ambazo hazijawajibika akitaka zifuate mfano wa Azima Sacco.

“Tungetaka serikali ifanye juhudi kuzidhibiti vyama vya ushirika vinavyokiuka sheria hasa kwa kufuja fedha za wateja wao huku wawekezaji wakiachwa na shida nyingi,” alisema Bw Mwangi.

Aliwataka wakuu wa vyama vya ushirika wawe waaminifu kwa wateja wao badala ya kufuja pesa zao kwa kujitajirisha wenyewe.