Vyombo vya habari vyatakiwa kuangazia habari za kilimo cha bayoteknolojia

Vyombo vya habari vyatakiwa kuangazia habari za kilimo cha bayoteknolojia

NA WANGU KANURI

VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuwekeza zaidi katika uandishi wa habari na makala kuhusu bayoteknolojia ili kutimiza azma ya utoshelevu wa chakula nchini.

Wakihutubu katika kongamano la ukuzaji wa vyakula kibayoteknolojia katika hoteli ya Nairobi Sports Club, wadau mbalimbali walisisitiz akuhusu haja ya wanahabari kuongeza juhudi katika uandishi wa mbinu za kilimo zinazotegemea bayoteknolojia.

Katika malengo yao wanasayansi wa mimea na wanahabari walijadili kuhusu mwongozo wa kinachopaswa kuripotiwa katika masuala ya kilimo.

Akichangia kupitia Zoom kutoka Nigeria, Diran Onifade, alisema kuwa wanahabari wanaporipoti masuala ya sayansi na ya bioteknolojia, wanapaswa kuhakikisha kuwa ukweli wa sayansi umekadiriwa.

Mhariri huyo wa masuala ya bayoteknolojia aliongeza kuwa ni hulka ya wanahabari kupata pande zote za ripoti kabla hawajaandika lakini kwa masuala ya sayansi na bayoteknolojia usawa huu wa pande zote ni vigumu kufikia.

“Unapojaribu kuhakikisha kuwa ripoti yako ina pande zote, unawashirikisha watu ambao si wataalamu ama wanasayansi. Kuwashirikisha watu ambao hawana ujuzi katika nyanja hizi ni kujenga uhakiki usio na msingi,” akaeleza Bw Onifade.

Kulingana naye, cha msingi sana kwa mwanahabari anayeripoti kuhusu masuala ya bioteknolojia na sayansi ni kuripoti mambo yaliyoidhinishwa.

Isitoshe, mwanahabari anapaswa kuhakikisha kuwa ameelewa pande za wanaohusika. Hawa ni watafiti, wanasayansi, wakulima na wasomi.

Walisema hiyo itahakikisha hujaegemea upande mmoja katika utafiti wako wa kuripoti. “Vile vile, wanahabari wanapaswa kueneza ujumbe waliokusanya kwa umma. Hata hivyo, ujumbe huu lazima uwe wenye lugha nyepesi na misamiati yakueleweka na mamia ya watu.”

Meneja wa mradi wa Jukwaa Wazi la Ukulima unaotumia Bayoteknolojia (OFAB), Vitumbiko Chinoko, alisema kuwa OFAB huwa kama daraja kati ya sayansi na wanaounda sera na watu kwa ujumla.

Malengo ya OFAB ni kuhakikisha kuwa kuna ushirikiano bora na ukulima wa bioteknolojia na washika dau mbalimbali.

Isitoshe, Bw Chinoko alishabikia kuwa kuna baadhi ya mafunzo ambayo wamejifunza kama shirika kwa kuangazia mazungumzo yanaoibuka katika mada ya ukulima unaotumia bioteknolojia.

“Sisi kama watu wanaounga mkono miradi inayoendeleza ukulima unaotumia bayoteknolojia, tunapaswa kuwasikiza wanaopinga miradi hii.

“Kilimo cha bayoteknolojia ni suluhu. Suluhu hii inalenga kuzimaliza shida za wakulima. Kwa mfano mkulima ambaye hawezi akapanda sababu kuna kiangazi, tunapaswa kuangazia vile teknolojia itamsaidia mkulima huyu akaweza kupanda na kuvuna mazao yake,” akaeleza Bw Chinoko.

You can share this post!

Magoha aapa kutetea CBC kwa hali na mali

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika shule ya...