Makala

Wa Amu wafurahia umaridadi wa jeti miaka 10 baadaye

May 3rd, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

UJENZI uliokuwa ukiendelea wa Jeti kubwa ya Mokowe, Kaunti ya Lamu umekamilika.

Jeti hiyo imekuwa ikijengwa kwa karibu miaka sita sasa.

Kukamilika kwake kumeleta afueni kwa mamia ya manahodha na wakazi wa kisiwa cha Lamu ambao wamevumilia miaka mingi ya mahangaiko wakitumia jeti kuukuu eneo hilo.

Jeti ni muundomsingi muhimu kwa uchukuzi wa baharini kwani ni kiunganishi cha pekee kwa watu au mizigo inayoshukishwa au kupandishwa kwenye boti na mashua kutoka au kuingia baharini.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Mhandisi Msimamizi wa Mradi huo, Bi Peace Oduk alisema mradi huo ambao una vipengee vitatu, vyote vimekalimika na kwamba kinachosubiriwa na hafla ya kukabidhi mradi kwa umma kufanyika.

Jumla ya Sh599 milioni zilitumika kwa ujenzi wa Jeti hiyo ya Mokowe.

Jumba la wasafiri kupumzika kuingia botini pamoja na vyoo vya umma kwenye jeti ya Mokowe, Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Inajumuisha Jeti yenyewe ya umma kutumia kwa shughuli zao za usafiri wa kila siku, jeti ya mafuta na jumba la wasafiri kusubiria, ikiwemo vyoo vya matumizi ya umma.

“Mradi umekamilika. Ulitekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi na Nyumba. Tuko tayari kuukabidhi mradi kwa umma wakati wowote,” akasema Bi Oduk.

Manahodha wa boti, mashua na jahazi, mabaharia na wakazi wa Lamu kwa jumla hawakuficha furaha yao baada ya jeti hiyo maridadi kukamilika.

Abdalla Twalib, nahodha tajika wa kisiwa cha Lamu, alitaja kukamilika kwa jeti hiyo kuwa mwamko mpya kwa sekta ya usafiri wa baharini.

“Twafurahia jeti yetu ya Mokowe. Ilijengwa kwa umaridadi kwelikweli. Tangu jadi hatujawahi kuwa na jeti yenye mahali pa wasafiri kupumzikia, vyoo vya kisasa na sehemu maalumu ambayo itatumika kama kituo cha mafuta jetini hapa. Twaishukuru serikali kwa juhudi zake kutuboreshea maisha,” akasema Bw Twalib.

Bi Barke Hussein alisema kujengwa upya na kukamilika kwa jeti kuu ya Mokowe ni hatua mwafaka itakayowapunguzia mahangaiko, hasa wasafiri akina mama ambao wamekumbwa na masaibu tele ya kutumia jeti kuukuu.

Bi Hussein anasema kumekuwa na visa vya akina mama kuteleza na kutumbukia baharini kwenye jeti ya zamani ya Mokowe.

“Muundo wa jeti ya zamani ulikuwa hauna reli ambazo angalau wasafiri wangekamata wanapopanda au kushuka kwenye jeti hiyo. Twashukuru jeti ya sasa ina sehemu kama hizo. Angalau sisi akina mama na watoto tuko salama,” akasema Bi Hussein.

Naye Bw Shariff Ali alisifu mtindo uliotumika kujenga jeti ya Mokowe na miradi tanzu yake.

Anasema mwonekano wa sasa wa Jeti kuu ya Mokowe umebadilisha mwonekano wa eneo hilo zima la forodha.

“Eneo la forodhani la Mokowe lote sasa ni jipya. Vipandevipande vya matofali (cabro) vimetandazwa vizuri. Kuna jengo jipya na la kifahari ambapo wasafiri hupumzika au kusubiriana nakadhalika. Yaani mambo hapa ni maridhawa kabisa,” akasema Bw Ali.

Mbali na jeti ya Mokowe, serikali kuu pia ilitekeleza ukarabati na upanuzi wa jeti nyingine za Lamu.

Ujenzi wa jeti hizo ulitekelezwa kati ya 2018 na 2023.

Miongoni mwa jeti hizo ni ile ya Mtangawanda iliyojengwa kwa kima cha Sh72 milioni, Jeti ya Lamu Mangrove kisiwani Lamu iliyokarabatiwa kwa kima cha Sh35 milioni ilhali jeti ya Uwanja wa Ndege wa Manda ikijengwa upya kwa kima cha Sh48 milioni.