Habari MsetoSiasa

Wa Iria ateua wataalamu kupiga msasa BBI

December 1st, 2019 1 min read

NA NDUNGU GACHANE

GAVANA wa Murang’a Mwangi Wa Iria ameteua kamati ya wataalamu ya watu 18 kupiga msasa ripoti iliyozinduliwa ya Jopokazi la Maridhiano(BBI) kisha kumwasilishia ripoti kuhusu masuala ambayo hajaangaziwa kwa muda wa wiki mbili zijazo.

Kulingana na kiongozi huyo, kamati hiyo inawahusisha wataalamu kutoka sekta za kibiasahara, viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu, wanauchumi, wafanyabiashara ndogondogo, wakulima na mashirika ya kijamii.

Wakati uo huo, Bw Iria aliwaomba viongozi wa kisiasa wasome ripoti ya BBI kwa kina kabla ya kutoa matamshi ya kuipinga au kuiunga mkono.

“BBI haikuafikiwa kupata uungwaji mkono au upinzani bali lengo lake kuu lilikuwa kuweka msingi na mwongozo wa kuyatatua matatizo mbalimbali nchini. Viongozi wanafaa kusoma ripoti hiyo kwa kina na kuhakikisha hoja ambazo hazikujumuisha zinawekwa ndani kwenye ripoti ya mwisho,” akasema Bw Iria.

Gavana huyo ambaye pia ni kinara wa Chama cha CRP aliwakashifu viongozi ambao wamegawanyika kuwili kuhusu iwapo ripoti hiyo inafaa kutekelezwa kupitia marekebisho ndani ya bunge au kupita kura ya maamuzi.

“Viongozi wetu wanawapoteza raia kwa sababu uamuzi wa mwisho kuhusu BBI unafaa kutolewa baada ya maoni ya raia kujumuishwa. Inasikitisha kwamba ripoti hiyo ilizinduliwa juma moja lililopita ilhali viongozi wanapigia upato au kuipinga hata kabla ya kuisoma,” akaongeza kiongozi huyo.

Aidha alifichua kwamba kama viongozi wa Mlima Kenya, wanasubiri kuandaa mkutano mwingine hivi karibuni na Rais Uhuru Kenyatta ambapo wataibua masuala yanayofaa kujumuishwa kwenye BBI kisha kuiunga mkono kama ripoti kamilifu itakayosuluhisha matatizo kadhaa ya eneo hilo.