HabariSiasa

Wa Muchomba atawataka wanaume kuoa wake wengi

April 3rd, 2018 2 min read

Na ERIC WAINAINA

MBUNGE Mwakilishi wa Kaunti ya Kiambu Gathoni wa Muchomba amewaomba wanaume katika jamii ya Agikuyu kuoa wake wengi, ili kuepuka matatizo yanayotokana na ulezi wa watoto bila baba zao.

Mbunge huyo alisema kuwa ukosefu wa wazazi wa kiume katika ulezi wa watoto umezua migogoro mingi ya kijamii miongoni mwa vijana, baadhi ikiwa kusambaa kwa ulevi.

Aidha, alisema kwamba wanaume ambao wanapata watoto na wanawake wengine wanapaswa kuwaoa kuwa wake wao halali, akishikilia kuwa kuwa na wake wengi si hatia ila ni suala la utamaduni.

Alikuwa akihutubu Jumatatu katika kituo cha Violence Recovery Centre, eneo la Wangunyu, Kaunti Ndogo ya Kiambaa, ambacho kinasimamiwa na afisi yake.

Alisema kuwa vijana wengi katika jamii hiyo ambao wamekuwa wakijiingiza katika ulevi na uhuni huwa wanafanya hivyo kwa kukosa malezi mema.
Kulingana naye, watoto wengi wa kurandaranda walio jijini Nairobi wanatoka katika jamii hiyo.

“Huwa tunapata watoto hao, ila huwa hatutaki kuwajibikia majukumu ya kuwalea. Ushauri wangu ni kwamba, ikiwa wewe ni mwanamume kutoka jamii ya Agikuyu, na una uwezo wa kuwaoa na kuwagharamia wake hadi watano, oa,” akasema.

Alisema kwamba jamii hiyo inapaswa kuweka kwenye mizani Imani yake ya kidini na utamaduni.

Kulingana naye, ikiwa kuoa wake wengi ndiko kutakuwa suluhusho la mgogoro wa sasa wa kijamii, basi kunapaswa kukumbatiwa kikamilifu na kukoma kuweka usasa mwingi katika masuala ya ulezi, akitaja hilo kama kiini kikuu cha changamoto za kijamii zinazoikumba jamii yake.

Waraibu wa pombe
Katika hafla hiyo, Bi Wamuchomba alizindua mpango wa kuwarekebisha tabia waraibu wa pombe, ambao utadumu kwa miezi mitatu. Alisema kuwa umma unapaswa kukumbatia suala hilo na kulitathmini kwa kina.

Alitaja kuwa kinaya hali ambapo vijana wengi waliofika katika hafla hiyo walikuwa wakiwataja mama zao kama wazazi wanaowajua.

“Hilo linaonyesha kwamba wanaume wengi hawajakuwa wakiwajibikia masuala ya ulezi. Huu ni mkasa mkubwa unaotukabili kama jamii,” akasema.

“Lazima tuwe wasema ukweli, Je, watoto wanaolelewa na akina mama wanazaliwa bila uwepo wa wanaume?” alishangaa.