Bambika

Wa Mumbi amulikwa kwa kupeleka nyayo nyingi ukweni

February 4th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MAPENZI kati ya maharusi, mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Betty Maina yamenoga kiasi kwamba hawaachani katika hafla za umma.

Hali ya Bw wa Mumbi kuandamana na mwakilishi huyo imeibua ucheshi na kejeli miongoni mwa mashemeji katika kaunti hizo mbili.

Kuna baadhi wanaomkumbusha Bw Wa Mumbi kwamba “uthoni ndurangarangagwo” kumaanisha “epusha nyayo nyingi kwa mashemeji au ukweni”.

Lakini videge hao wanasema hali yao ni tofauti kwa kuwa ni viongozi walio katika huduma.

Akiwa katika mahojiano ya runinga ya Inooro hivi majuzi, Bw wa Mumbi alisema “kwa kweli Betty yuko sawa, tuko pamoja na tunazidi kusukumana kimaisha”.

“Kwa kuwa Bi Maina ni mama wa Kaunti ya Murang’a, sasa ni lazima nami nitembee naye kama baba wa Kaunti,” Bw wa Mumbi alisema.

Kwa upande wake, Bi Maina ameshikilia kwamba wako katika ile hali ambayo nd’o kwanza utamu unakolea.

“Tunalea watoto wetu pamoja licha ya kuwa hatuna mipango kwa sasa ya kuongeza wengine,” akasema Bi Maina.

Alisema ndiyo wanafahamiana kwa undani kabisa na kwa sasa amejifunza mengi.

“Nimegundua huyu ni mwanamume mzuri wa kawaida asiye na mambo mengi… bora tu nimwandalie kuku wa kuchemshwa aliyewekwa viazi kwa utumbo,” akasema.

Aliongeza kwamba kubadilisha mlo, “Wa Mumbi hupenda ‘mukimo wa njahi ambapo huwa ninakaanga.”

Hivi majuzi, Bi Maina alimshambulia mwandishi wa habari mmoja wa eneo la Mlima Kenya kwa madai kwamba alifichua kuhusu hundi ya pesa zilizonuiwa kuwa za Mathira kupeanwa katika mradi wa Murang’a.

Bi Maina hakufurahishwa hata kidogo na madai hayo.

[email protected]