Habari Mseto

Waathiriwa wa 2007/8 kortini kutolipwa fidia baada ya kushinda kesi

July 3rd, 2019 1 min read

JOSEPH OPENDA na KATE WANDERI

WAATHIRIWA 69 wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 ambao walishinda kesi ya kudai fidia kutoka kwa serikali, wamerudi kortini kushtaki idara za serikali kwa kutotii maagizo ya mahakama.

Wakimbizi hao wa ndani kwa ndani wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Nakuru wakilaumu makatibu wa wizara za ugatuzi na fedha kwa kukaidi maagizo yaliyotolewa kwao kuwalipa Sh2.5 milioni kisha kuwapa makao mapya kwenye ardhi ya ekari 155.

Kulingana na uamuzi uliotolewa na Jaji Maureen Odero (pichani) 2016, serikali iliagizwa kulipa kila mmoja wao Sh35,000 na kuwapa ardhi ya ekari 2.25 kila mmoja.

Hata hivyo, walalamishi walidai serikali haijatekeleza agizo hilo miaka mitatu baadaye na juhudi zao kufuatilia suala hilo hazijafua dafu.

Kupitia kwa wakili wao Wilfred Konosi, walalamishi wanataka agizo litolewe kulazimisha serikali iwalipe.

Walalamishi hao 69 kutoka Kuresoi, kaunti ya Nakuru walienda mahakamani 2015 kushtaki serikali kwa kuwatenga ilipolipa IDP wengine fidia.

Walidai waathiriwa wa ghasia zilizotokea nchini 2007 kufuatia matokeo tatanishi ya uchaguzi wa urais kati ya aliyekuwa rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambapo watu zaidi ya 1,000 waliuawa na maelfu wengine wakaachwa bila makao.

Kupitia kwa hati ya kiapo ya Bw Peter Nyakundi kwa niaba ya wengine 68, walidai serikali iliwabagua wakati IDP wengine 278 walilipwa fidia.

Bw Nyakundi alisema kuna IDP 206 ambao walipewa Sh10,000 kuanzisha maisha upya, Sh25,000 kujenga nyumba upya na ardhi za ekari 2.25 kila mmoja.

Mahakama ilitambua kwamba walalamishi hao walikuwa na haki ya kulipwa ridhaa sawa na jinsi wengine waliokuwa wamekimbilia kambi ya Saw Mill iliyokuwa Molo walivyolipwa.

Kesi hiyo ilipotajwa mahakamani jana ilibainika serikali haijatoa majibu yake. Jaji Joel Ngugi aliagiza suala hilo litajwe Julai 10.