Habari Mseto

Waagizaji magari wasema huduma za SGR ni ghali

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WAAGIZAJI bidhaa kutoka nje ya nchi wamependekeza kuongezwa kwa ada ya maendeleo ya reli (RDL) kutoka asilimia 1.5 za sasa hadi asilimia tatu.

Pia walipendekeza kukubaliwa kutumia njia zingine za kuchukua mizigo yao zaidi ya Reli ya Kisasa (SGR) ambayo walisema ina gharama ya juu.

Chama cha Waagizaji wa Magari Madogo nchini (CIAK) kupitia kwa mwenyekiti wao Peter Otieno walisema waagizaji wamo tayari kulipa adqa zaidi ili wakubaliwe kusafirisha mizigo yao kwa njia wanayopenda kuliko kulazimishwa kutumia SGR na depo ya ndani Nairobi (ICD), ambayo walisema imewaletea changamoto nyingi.

Walipendekeza hayo wakati ambapo Mamlaka ya Bandari (KPA) imetoa notisi kwa kampuni za uchukuzi wa majini na maajenti wao kukoma kupendekeza uchukuzi wa pamoja wa bidhaa nyingi katika vituo vya uchukuzi wa kontena (CFSs).

Hii ina maana kuwa mchele, mbolea, mafuta, vifaa, nguo za mtumba na lami zitasafirishwa hadi depo ya ndani Nairobi, hali inayotarajiwa kuzua changamoto zaidi.

Kulingana na Meneja Mkurugenzi wa KPA Dkt Daniel Manduku, serikali imeanzisha mikakati kuimarisha uchukuzi wa bidhaa na mizigo bandarini na depo ya Nairobi.

Lakini waagizaji wa magari madogo walipinga hilo kwa kusema kuhamishiwa kwa mizigo zaidi ICD kutaibua msongamano zaidi na kusababisha kucheleweshwa kwa mizigo kufikia wenyewe hasa kutokana na kuwa tayari msongamano unashuhudiwa katika depo hiyo.