Habari Mseto

Waajiri wahimizwa wafidie waandishi wanapovamiwa

September 4th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

ASASI za kusimamia waandishi wa habari nchini zimehimizwa kuhakikisha wanahabari wanalipwa ridhaa wanaposhambuliwa ama vifaa vyao kuharibiwa wakiwa kazini.

Akihutubu Jumatno kwenye ufunguzi wa Kongamano la Wanahabari Kuhusu Ugatuzi jijini Nairobi, aliyekuwa Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Nyeri Bi Priscilla Nyokabi alisema kwamba, wanahabari wengi hawajakuwa wakilipwa ridhaa wanaposhambuliwa, licha ya masaibu yao kuangaziwa.

Alisema asasi za kuwatetea kama Baraza la Vyombo vya Habari Kenya (MCK) hazijakuwa zikichukua hatua za kutosha kutetea maslahi ya wanahabari, licha ya kukashifu mashambulio dhidi yao.

“Licha ya MCK kujitokeza kuwatetea sana wanahabari, juhudi zaidi zinahitajika katika kuhakikisha wanalipwa ridhaa ikiwa wanajeruhiwa ama vyombo vyao kuharibiwa,” akasema Bi Nyokabi.

Visa vya wanahabari kushambuliwa na kujeruhiwa ama vyombo vyao kuharibiwa wakiwa kazini vimekuwa vikiongezeka, hasa katika kiwango cha kaunti.

Baadhi yao hata wameuawa katika hali tatanishi, huku waliohusika katika visa hivyo wakikosa kuchukuliwa hatua.

Mwaka uliopita, mwanahabari Barack Oduor wa Shirika la Habari la Nation (NMG) alinusurika kifo, baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana pamoja na mwanadada Sharon Otieno katika Kaunti ya Homa Bay, ambapo baadaye msichana huyo alipatikana akiwa ameuawa.

Mnamo Juni, wanahabari wa shirika la habari la Standard Group Carolyne Bii, Boniface Magana (mpiga picha) na Immaculate Joseph (dereva) walinusurika kifo baada ya gari lao kushambuliwa na kuchomwa na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya St Joseph’s katika Kaunti ya Machakos.

Kulingana na Bi Nyokabi, asasi zilizopo hazijakuwa zikizingatia sheria kuhakikisha wanahabari wanaojipata matatani wanalipwa ridhaa kutokana na hasara wanayopata.

“Kuna sheria inayoeleza jinsi wanahabari wanaoshambuliwa wakiwa kazini wanapaswa kulipwa ridhaa kwa hasara wanayopata,” akasema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Kandarasi (KCA) William Janak alisema kuwa, tangu Januari, wamepokea visa 38 vya wanachama wao ambao wameshambuliwa wakiwa kazini.

Alisema wameanza mikakati ili kushinikiza asasi husika kuchukulia kwa uzito na kufuatilia visa vya wanahabari wanaoshambuliwa.