Michezo

Waalgeria waitania Kenya kujumuisha mshambuliaji Masud timu ya Harambee Stars

October 1st, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa timu ya JS Kabylie na Algeria wamefungua roho kuchekelea Kenya kwa kujumuisha mshambuliaji Masud Juma katika kikosi cha Harambee Stars kitakachopepetana na Sudan/Libya (Oktoba 9) na Zambia (Oktoba 12).

Stars itatumia michuano hiyo ya kirafiki kujipiga msasa kabla ya kugaragazana na wanavisiwa wa Komoro nyumbani (Novemba 9) na ugenini (17) katika mechi mbili zijazo za Kundi G za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Baada ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kutangaza kikosi cha wachezaji 34 hapo Septemba 28, JS Kabylie ilichapisha ujumbe na picha ya Juma uliosema:

“Masud Juma Choka ameitwa katika timu ya taifa ya Kenya kushiriki mechi mbili za kirafiki. Mechi ya kwanza imeratibiwa kusakatwa Oktoba 9 dhidi ya Sudan ama Libya halafu ya pili itakuwa Oktoba 12 dhidi ya Zambia. Juma ataungana na timu hiyo ya Kenya hapo Oktoba 5 na anatarajiwa kurejea nchini Algeria mnamo Oktoba 13.”

Mashabiki kutoka Algeria walichangamkia ujumbe huo. Avahri Thili alisema, “Maskini soka! Hakucheza hata dakika moja msimu uliopita. Inakuwaje anajumuishwa katika timu ya taifa.”

Lyes Kasdi, “Labda amejumuishwa kwa timu ya riadha kwa sababu katika kipindi cha miaka miwili amekuwa hapa, hajatuchezea zaidi ya mechi tatu.”

Malik Va ßeñe Dafeur, “Kweli, huwajakosea kukujumuisha katika timu ya riadha. Kila la kheri. (Bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 1,500 mwaka 2012) Toufik Makhloufi kaa chonjo utapoteza medali yako ya dhahabu.”

Messaoudi Ayoub, “Sielewi kwanini bado huyu Juma yuko katika kikosi chetu cha JS Kabylie. Hastahili kuwa hapa…”

Midou Pirlo, “Maskini Bara Afrika, maskini JS Kabylie. Mchezaji huyu amekuwa katika chumba cha majeruhi msimu wote. Inashangaza kuwa anaitwa katika timu ya taifa na hajafunga bao lolote wala kusakata mechi moja nzima.”

Hachemi Ab, “Ni aibu kubwa kuwa bado baadhi ya mataifa ya Afrika yanafanya vitu kama hivi.”

Vødk? Põmmë, “Sijawahi kuona mchezaji ambaye hachezei klabu yake halafu anajumuishwa katika timu ya taifa.”

Mhand Djebarra, “Tunatumai atatuonyesha uwezo wake jinsi tulivyoona kwenye video zake kwa sababu kufikia sasa hajatufanyia chochote hapa.”

Kalif Achet, “Pongezi kwake na kila la heri tukitumai kuwa mwaka huu hataandamwa na majeraha.”

Juma alijiunga na Kabylie mnamo Julai 25 mwaka 2019 kutoka Al-Nasr Benghazi nchini Libya kwa kandarasi iliyofaa kukatika Juni 30, 2020.

Alichezea Kabylie mechi 10 ligini na mbili kwenye Klabu Bingwa Afrika msimu 2019-2020 ikiwemo dhidi ya ES Setif kwenye Ligi Kuu ya Algeria mnamo Machi 15, ambayo ilikuwa ya mwisho kabla ya janga la virusi vya corona kukatiza msimu huo.

Kabylie ilirejelea mazoezi baada ya miezi sita mapema mwezi Septemba. Mnamo Septemba 18, iliripotiwa kuwa Juma alihofiwa kupatikana na virusi hivyo. Aliingia karantini siku 12. Mnamo Septemba 27, alichapisha ujumbe akishukuru waliomtakia afueni ya haraka. Alieleza kuwa haelewi corona inavyokaa kwa sababu alipopimwa Septemba 18 alipatikana na virusi hivyo halafu Septemba 22 hakuwa navyo.

Juma amewahi kuchezea Kenya mara tatu na pia alikuwa katika kikosi cha kocha Sebastien Migne kilichoshiriki AFCON 2019.

Komoro inaongoza Kundi G kwa alama nne baada ya kuchapa Togo 1-0 mjini Lome na kulazimisha sare tasa dhidi ya Misri mjini Moroni. Kenya na Misri zinafuatana katika nafasi ya pili na tatu mtawalia kwa alama mbili. Vijana wa kocha Francis Kimanzi walikaba Misri 1-1 mjini Alexandria kabla ya kukubali sare kama hiyo dhidi ya Togo uwanjani Kasarani. Togo inavuta mkia kwa alama moja.