Michezo

Waamuzi 8 wa Kenya kunolewa kuhusu takwimu za vipaku

June 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KENYA kwa sasa itakuwa na wataalamu wa takwimu wa kiwango cha kimataifa kwenye mchezo wa vikapu baada ya waamuzi wanane kuteuliwa kushiriki mafunzo maalumu wiki ijayo kwa udhamini wa Shirikisho la Vikapu la Afrika (FIBA).

Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF), Ambrose Kisoi amesema mafunzo hayo yatakayoendeshwa mtandaoni kwa siku mbili, yatakuwa hatua kubwa katika maendeleo ya mpira wa vikapu humu nchini.

Watakaoshiriki mafunzo hayo kikamilifu watakuwa na fursa ya kunakili takwimu za mechi za kiwango cha kimataifa ndani na nje ya Kenya.

“Kenya haijawahi kuwa na waamuzi ambao ni wataalamu wa kimataifa wa takwimu walioidhinishwa na FIBA. Hii ni fursa maridhawa kwa watakaoshiriki mafunzo haya kuchangia maendeleo ya mchezo huu humu nchini,” akasema Kisoi.

Wakati wa mechi za kufuzu kwa fainali za FIBA Africa Zone Five zilizoandaliwa Nairobi mnamo Januari mwaka huu, FIBA ililazimika kumtafuta mtaalamu wa takwimu za vikapu kutoka Uganda.

Kati ya watakaofunzwa wiki ijayo kuhusu jinsi ya kuchukuwa takwimu, ni Patrick Odhiambo na Eddy Kalume wa Ulinzi Warriors, Teddy Amino, Nelly Odera, Sylvia Ongwae, Mary Makau, Gertrude Sagala na Rodreque Wanyama.

Kenya imetiwa katika Kundi C kwa pamoja na Zimbabwe, Tanzania, Sudan Kusini, Algeria, Equatorial Guinea, Libya, Rwanda, Algeria na Guinea Bissau kwenye fainali za FIBA Africa Zone Five.

Kwingineko, wanavikapu wa Kenya Morans watafungua kampeni za Kundi B za kuwania taji la Afrika FIBA AfroBasket mnamo Novemba 27 kwa kuvaana na Senegal.

Moranas watapepetana na Angola mnamo Novemba 28 katika mchuano wao wa pili kabla ya kufunga mechi za makundi dhidi ya Msumbiji mnamo Novemba 29.

Mkondo wa pili ya kipute cha AfroBasket umeratibiwa kuanza Februari 19, 2021 kwa mechi itakayowakutanisha tena Kenya na Senegal. Baadaye, watashuka ugani kukabiliana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Msumbiji mnamo Februari 22.

Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya kimataifa, Morans ndio wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wanashikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.

Jumla ya vikosi 20 vitapangwa katika makundi matano ya vikosi vinne kwa minajili ya mechi za raundi ya pili ya mchujo. Washindi watatu wa kwanza kutoka kila kundi watajikatia tiketi za kushiriki fainali za FIBA AfroBasket zitakazoandaliwa jijini Kigali, Rwanda.

Chini ya kocha Cliff Owuor, Kenya inalenga kunogesha fainali za kipute hicho cha haiba kubwa barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1993.

ReplyForward