Kimataifa

Waandamana uchi kupinga mamilioni ya wanyama kuuawa ili kuunda mavazi

December 20th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

Barcelona, Uhispania

WANAHARAKATI wa kutetea haki za wanyama pori walitekeleza maandamano wakiwa uchi na kujipaka damu, wakieleza pingamizi zao kuhusu matumizi ya manyoya na ngozi kwa nguo.

Makumi ya wanaharakati hao walivua nguo zote na kusalia uchi wa mnyama, huku wakilala katika bustani moja ya kitalii mjini Barcelona, Uhispania kando ya kibao kilichoandikwa “ni wanyama wangapi huuawa kuunda koti moja tu?”

Maandamano hayo yaliandaliwa na kikundi cha watetezi wa haki za wanyama cha Anima Naturalis, tawi la Uhispania.

Picha zilizosambaa mitandaoni duniani kote zilionyesha wanaharakati hao wakilala katika kikundi, huku mili yao iliyokuwa uchi ikipakwa damu. Walisisitiza kuwa jamii inafaa kufahamu “unyama ilioko ndani ya viwanda vya nguo”

Wanaharakati hao walidai kuwa wanyama milioni 32 huchinjwa barani Uropa kwa ajili ya ngozi kila mwaka.

Ripoti za vyombo vya habari nchi hiyo, wanaharakati hao walitaka kupaza sauti kwa niaba ya mamilioni ya wanyama ambao wanauawa kwa ajili ya biashara.

Mwaka uliopita, wanaharakati wa kikundi hicho waliandamana bila mavazi ya juu ya mwili, wakivalia pembe na kujipaka damu feki katika mitaa ya Pamlona, kama njia ya kupinga mashindano ya mbio za ndume kila mwaka.

Waliandamana wakirusha vumbi nyekundu hewani kama njia ya kuonyesha kuwa mashindano hayo, ambayo yalivutia maelfu ya watu, hayakuwa na maana.

Wanaharakati hao wamekuwa wakitekeleza maandamano hayo kwa miaka 14 ambayo imepita.