Waandamanaji wakabiliana jijini Kisumu

Waandamanaji wakabiliana jijini Kisumu

WATU wengi wamejeruhiwa na dirisha la gari la polisi kuvunjwa kwa mawe baada ya makundi mawili ya kisiasa kuvurugana jijini Kisumu, Jumapili.

Ghasia zimeanza baada ya kundi moja la watu wachache kuandaa maandamano ya amani kutaka sheria izingatiwe na viongozi wakuu nchini wakumbatie mazungumzo kuhusu masaibu yanayokumba nchi.

Hata hivyo, wamevamiwa na kulishwa kichapo na umati ambao unaunga mkono maandamano yatakayoongozwa na Kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kesho Jumatatu.

Imebidi waandamanaji walionekana kupinga msimamo wa Bw Odinga kutawanyika na kukimbia ili kujinusuru kutokana na uvamizi huo.

Aidha polisi ambao walioingilia kati kutuliza maandamano hayo nao wamepigwa kwa mawe huku wakilazimika kuwaleta wenzao zaidi. Hata hivyo, waandamanaji hao wamesisitiza kwamba Jumatatu watakuwa barabarani kama njia ya kusimama na Bw Odinga ambaye ni kigogo wa siasa za eneo hilo.

“Hatuwezi kuwaruhusu watu ambao wamelipwa waje hapa watuchokoze. Sisi tutaandamana Jumatatu kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha,” amesema mkazi wa Nyalenda Stephen Okumu.

Wamemkosoa Seneta wa Kisumu Profesa Tom Ojienda kwa kudhamini maandamano ya kundi pinzani na kumtaka ajiuzulu wadhifa wake iwapo anaona umaarufu wake umepanda kuliko wa Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Linturi aonya wakora wanaouza mbolea ya serikali

Jennifer Kananu Mbogori ni mwasisi wa kampuni ya...

T L