Maoni

Waandamanaji walivamia Bunge Amerika na hakuna mtu aliuawa!

Na DOUGLAS MUTUA June 28th, 2024 2 min read

BUNGE la Kenya linavamiwa kwa dakika chache tu, raia zaidi ya 10 wanauawa! Bunge la Amerika linavamiwa siku nzima, afisa mmoja wa polisi pekee anauawa. Shida yetu Kenya huwa gani? Yaani kuua mtu kumekuwa rahisi hivyo?

Katika kisa cha Kenya, wavamizi wachache tu wanakamatwa na polisi na kupandishwa kizimbani.

Maelfu ya waliovamia Bunge la Marekani wanashtakiwa, baadhi yao wanafungwa jela. Waliokwenda mafichoni wanatafutwa miaka minne baadaye.

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye aliwachochea wavamizi hao, anachunguzwa na huenda akashtakiwa wakati wowote kutokana na jukumu hilo alilotekeleza, ambalo ni kosa la jinai.

Ukiangalia visa hivyo viwili, unatambua kuwa mbinu mbili tofauti zilitumika kushughulikia tatizo la uvamizi wa maeneo hayo muhimu ya Bunge.

Ingawa kote kuwili lugha inayotumiwa ni kwamba uvamizi uliofanywa ulihatarisha usalama wa kitaifa, unatambua kwamba uhai wa mwanadamu una thamani tofauti kutegemea uko wapi.

Nchini Marekani, ni heri polisi afie kazini akijaribu kuwazuia raia kutenda uhalifu. Afisa aliyeuawa katika kisa hicho alibanwa kwa mlango akiwakataza wavamizi kuingia ndani ya Bunge.

Nchini Kenya, polisi wanafyatua risasi za shaba hata kabla ya wavamizi kuwakaribia. Haiwi kwao ni tatizo kuua mtu wakiwa kazini kwa sababu wanajua hawatachukuliwa hatua yoyote.

Kumbuka shirika linalowatetea raia dhidi ya dhuluma za polisi (IPOA) ni jibwa kibogoyo lisilong’ata yeyote, hivyo hakuna anayeliogopa.

Mtazamo wa polisi wa Amerika ni kwamba, wananchi waliokuwa na hasira walivamia jengo lao.

Kwamba walitenda uhalifu kwa kufanya hivyo ni suala ambalo linaweza kushughulikiwa kisheria pasina mtu kuuawa na polisi.

Nchini Kenya, ni dhambi kuingia jengo wanamoketi waheshimiwa, watu na hadhi zao, hivyo ukikutana na risasi katika shughuli hiyo jilaumu mwenyewe.

Na hali ikiwa mbaya zaidi watu wenu wakuandalie mazishi wiki ijayo! Ukiwa Mwislamu utazikwa saa 24 baadaye.

Katika kisa cha Amerika, suala la mfumo unaotenda kazi inavyostahili linajitokeza. Kila taasisi inawajibika inavyostahili.

Polisi wanaojipata katika eneo la tukio wanajua vyema kwamba wao si waamuzi wa mwisho katika kisa kile.

Wanajua ni makosa kwao kutekeleza majumu ya polisi anayemkamata mshukiwa, mchunguzi wa jinai, jaji na mtekelezaji hukumu inayotolewa. Kila mtu anatenda kazi yake.

Nchini Kenya, afisa wa cheo kidogo sana cha konstebo anaweza kutumia bunduki kubwa ya AK47 kukusindikiza mpaka kaburini, lako liwe tu kusubiri siku ya kiyama wafu watakapofufuliwa na hukumu ya mwisho itolewe na Mwenyezi Mungu.

[email protected]