Michezo

Waandishi wamchagua Henderson mchezaji bora wa msimu EPL

July 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO na nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson ametawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa kitengo cha tuzo za wanadimba wa kiume za Chama cha Waandishi wa Soka.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 aliwaongoza Liverpool kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya miaka 30 ya kusubiri. Henderson alijizolea zaidi ya robo moja ya kura zilizopigwa.

“Sioni kabisa kustahiki kwangu, ila tuzo hii ni zao la mchango mkubwa kutoka kwa watu wengi. Ni tuzo ambayo naitabarukia timu nzima ya sasa ya Liverpool. Kikosi kimekuwa thabiti na imara na kudhihirisha kiu ya kusajili ushindi katika takriban kila mchuano wa muhula huu,” akasema Henderson wakati wa kupokea tuzo hiyo.

Wansoka Virgil van Dijk na Sadio Mane wa Liverpool pamoja na kiungo Kevin De Bruyne wa Manchester City na Marcus Rashford wa Manchester United ni miongoni mwa wanasoka wengine waliokuwa wawaniaji wa tuzo hiyo. Wote hao waliibuka katika orodha ya tano-bora. Mnamo Julai 22, Henderson ambaye bado anauguza jeraha la goti, alipokezwa kombe la EPL msimu huu kutoka kwa nguli wa soka kambini mwa Liverpool, Sir Kenny Dalglish uwanjani Anfield.

“Napokea tuzo hii kwa niaba yangu binafsi na wanasoka wote wa kikosi cha Liverpool. Bila wao, nisingeweza kabisa kutwaa ubingwa huu. Wenzangu kambini mwa Liverpool wameniwezesha kuwa mwanasoka bora zaidi, kiongozi bora zaidi na mtu bora zaidi. Naamini kwamba wote walionipigia kura walifanya hivyo katika juhudi za kutambua mchango wa kikosi kizima katika kuniboresha hadi kufikia nilipo na nilivyo kitaaluma,” akaongeza Henderson.

Henderson aliwaongoza Liverpool pia kunyanyua taji la Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia mnamo Disemba 2019.

Nje ya uwanja, Henderson amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanasoka wenzake wa EPL kuchangisha fedha kwa minajili ya Hazina ya Kitaifa ya Afya katika juhudi za kukabiliana na janga la corona kupitia mradi wa #PlayersTogether.

Mvamizi wa Arsenal na timu ya taifa ya Uholanzi, Vivianne Miedema alitawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake.