Habari Mseto

Waandishi wataka haki kwa Dotto Rangimoto

October 5th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

KUNDI la waandishi limekosoa vikali kuzuiliwa kwa naibu afisa wa mawasilianao wa chama cha ACT Wazalendo, Dotto Rangimoto, wakiitaka Serikali ya Tanzania kumwachilia huru au kumpeleka kortini.

Kupitia taarifa iliyoonekana Jumapili na Taifa Leo, kundi hilo linaitaka serikali ya Rais John Pombe Magufuli kumwachilia huru afisa huyo au kumwasilisha kortini kuambatana na sheria.

Aidha, kundi hilo linalojiita Washiriki wa Tuzo ya Kiswahili ya Fasihi za Kiafrika Mabati – Cornel, limeshutumu mamlaka nchini humo dhidi ya kukiuka sheria inayokataza mshukiwa yeyoye kuzuiliwa kwa zaidi ya saa 24 pasipo kufikishwa kortini.

“Kwa umoja wetu, sisi wanafasihi ambao tuliwahi kuwa katika orodha za washiriki wa Tuzo za Kiswahili za Fasihi ya Afrika za Mabati-Cornell, tunaziomba mamlaka husika ama kumuachilia huru Dotto Rangimoto au kumpeleka mahakamani kwa mujibu wa sheria za nchi, ambazo zinakataza mtu yeyote kuwa chini ya mikono ya vyombo vya dola kwa zaidi ya saa 24 bila kushtakiwa,”

“Tunaomba kama lipo ambalo anatuhumiwa kwalo, basi mchakato wa kesi yake uendeshwe kwa haki na kwa dhana kwamba hana makosa kwa mujibu wa sheria hadi pale mahakama itakapoamua vinginevyo,” ilisema taarifa hiyo.

Pia wasomi hao wamedai kuwa afisa huyo amenyimwa haki zake za kibinadamu na kisheria kwa kuzuiwa kuonana na jamaa au hata mawakili wake, tangu alipokamatwa karibu wiki mbili zilizopita.

“Sisi washiriki wa tuzo tajwa hapo juu, tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa habari za kushikiliwa mshiriki mwenzetu, Bwana Dotto Rangimoto, na Mamlaka nchini Tanzania katika namna ambayo tunaamini inavunja haki zake za kisheria na pia za kibinadamu,”

“Tokea tarehe 25.09.2020, Bwana Dotto Rangimoto yuko mikononi kwa vyombo vya dola, ambako, kwa mujibu wa taarifa tunazopokea haruhusiwi kuonana na ndugu wala wanasheria wanaomuwakilisha,” walisema.

Haya yamejiri karibu wiki mbili tangu Bw Rangimoto kukamatwa mnamo Septemba 25, 2020 pamoja na maafisa wenzake wawili katika chama hicho,

Hata hivyo, maafisa hao, Bi Arodia Peter, afisa wa mawasiliano katika chama na Bi Dahlia Majid mkurugenzi wa kampeni za kimataifa waliachiliwa baadaye huku Bw Rangimoto akiendelea kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

Kulingana na naibu katibu wa Maarifa na Mawasiliano ya Umma katika chama hicho Bi Janeth Rithe, Bw Rangimoto alikamatwa kuhusiana na tuhuma za kukiuka Sheria kuhusu Uhalifu Kimtandao.

Maafisa wenzake walioachiliwa baadaye walikuwa wamekamatwa kwa kosa la kuwazuia maafisa wa usalama kufanya kazi yao,