Kimataifa

Waasi wa M23 wadhibiti eneo la madini ya kutengenezea smartphone

May 2nd, 2024 2 min read

NA REUTERS

KINSHASA, DRC

WAASI wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameudhibiti mji wa Rubaya, ambao ni muhimu kwa uchimbaji wa madini aina ya coltan yanayotumika kutengeneza simu za smartphone, msemaji wa waasi amesema.

Hii ni kufuatia siku kadhaa za mapigano makali.

Eneo la mashariki mwa DRC limekumbwa na ghasia tangu miaka ya tisini (1990s), hali ambayo imesababisha vifo vya mamilioni ya watu katika vita vya kutaka utambulisho wa kitaifa, ukabila na kung’ang’ania rasilimali.

Baadhi ya mataifa jirani yanalaumiwa kwa kujiingiza kwa mkwamo huo ambao umesababisha makundi ya waasi wenye silaha kuchipuka.

Willy Ngoma, msemaji wa jeshi la M23 ambalo inadaiwa wanachama wake wengi ni Watutsi, aliambia shirika la habari la Reuters kuwa mji huo wa wa eneo la Kivu Kaskazini ulikuwa chini ya udhibiti wao baada ya kuyafurusha makundi mengine yenye silaha katika eneo hilo, likiwemo lile la Forces for the Liberation of Rwanda, ambalo inadaiwa wanachama wake wengi ni Wahutu.

Msemaji wa jeshi la DRC kuhusu operesheni dhidi ya M23, Luteni Kanali Guillaume Njike, alisema hawawezi kuthibitisha uhalisia wa madai hayo.

“Tunaendelea na uchunguzi kuanzia jana (Alhamisi) kubaini iwapo mji huo uko chini ya udhibiti wa waasi wa M23,” Njike aliambia wanahabari.

Utajiri mkubwa wa madini nchini humo uko katika eneo la mashariki, ambalo limeshuhudia hali ya utovu wa usalama tangu kundi la M23 liliporejelea mashambulio mnamo Machi 2022.

Mji wa Rubaya uko na utajiri mkubwa wa madini ya tantalum, yanayotolewa kutoka coltan, na ambayo ni madini yanayotumika katika utengenezaji wa simu za rununu, tarakilishi, miongoni mwa mitambo mingine ya kieletroniki.

Kundi la M23 limewahi kuchukua udhibiti wa mji huo mara mbili, kwa siku chache, tangu lilipoanza mapigano yake mapya.Serikali ya DRC, maafisa wa Umoja wa Mataifa (UN) na mataifa ya Magharibi yameishutumu Rwanda kwa kutoa usaidizi kwa kundi hilo la waasi, madai ambayo Rwanda imekana mara kadha.

Kiongozi wa kundi moja la vijana katika mji huo wa Rubaya aliambia Reuters kwa simu kwamba umezingirwa na waasi hao.

“Watu wengi wametoroka kwa sababu mapigano ni makali,” Clovis Mafare akasema na kuongeza kuwa wachimba madini pia wametoroka.

Awali, mji wa Rubaya ulikuwa chini ya udhibiti wa kundi la wapiganaji, linalounga mkono serikali ya DRC, kwa jina Wazalendo.

Umoja wa Mataifa ulisema Desemba 2023 kwamba kundi la Wazalendo lilidhibiti ya kuchimba na kusafirisha madini kama vile “tin”, “tantalum” na “tungsten”.

Mapigano yamewahi kuzuka kuhusu udhibiti wa biashara haramu ya madini ya “tin”, dhahabu, “coltan” na “tantalum” yanayochimbwa DRC kabla ya kusafirisha kupitia nchi jirani za Rwanda, Uganda, na Burundi.