Habari za Kaunti

Waathiriwa wa mafuriko Juja wapokea misaada ya kiutu

May 18th, 2024 1 min read

NA LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Zetech kimeshirikiana na mashirika mengine mawili kuwapa misaada ya chakula waathiriwa wa mafuriko eneo la Juja katika Kaunti ya Kiambu.

Mashirika hayo yaliyojitolea kushirikiana na chuo hicho ni vuguvugu la vijana la Crime si Poa, na Oshwal Mahila Mandal.

Familia 150 zilifurika katika Zetech University Technology Park eneo la Mang’u kupokea misaada.

Walengwa walipokea mablanketi, chakula na miavuli.

Baada ya kupokea misaada hiyo, wananchi hao walishauriwa kuvitumia kwa umakini bila kuuza tena kwa manufaa ya kifedha.

Baadhi ya maafisa wakuu waliohudhuria hafla hiyo ni mkurugenzi wa uhusiano mwema wa Zetech Bw John Mwai, mkurugenzi wa uhusiano mwema na soko Dkt Beauttah Mwangi, mkurugenzi wa Zetech Bw Peter Ouko, mkurugenzi wa shirika la Crime si Poa, na Bi Bharti Raja, ambaye ni mwenyekiti wa wanawake wa Oshwal Mahila Mandal.

Wakurugenzi hao walipongeza juhudi waliofanya ya kujali jamii zilizoathirika.

Waathiriwa wa mafuriko eneo la Juja katika Kaunti ya Kiambu wasikiliza hotuba kabla ya kupokea misaada ya kiutu. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Bw Mwai alitilia mkazo umuhimu wa Zetech kuchukua jukumu la kuwajali waathiriwa.

“Kila mara sisi tuko tayari kusaidia jamii zinazoathirika kwa njia moja au nyingine. Tutafanya tuwezalo kuona tunafaulu katika mipango hiyo,” alisema Bw Mwai.

Naye Bi Raja alipongeza ushirikiano wa pamoja wa kuwasaidia wanajamii waliopata shida ya mafuriko.

“Sisi ni watetezi wa wanawake tunafurahi kushirikiana na Zetech ili kujali jamii zinazohitaji misaada,” alieleza Bi Raja.

Alisema ushirikiano huo wa pande zote tatu unastahili kuendelezwa kwa pamoja bila kulegeza kamba.

“Ushirikiano huo utaendelezwa zaidi ili jamii ziendelee kupata misaada bila kulegeza kamba,” aliongeza.

Wakurugenzi hao walielezea umuhimu wa ushirikiano huo wa pamoja na kuhakikisha jamii hizo hazipati shida wakati wowote kunapotokea janga.