Habari Mseto

Waathiriwa wa mafuriko wasaidiwa

April 27th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WATHIRIWA wa mafuriko katika Kaunti ya Homa Bay wameanza kupewa pesa ili waweze kukodisha nyumba waache kukusanyika katika kambi.

Hayo yanajiri huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ikisema mvua kubwa inayosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi sehemu nyingi za nchi itaanza kupungua Mei 1.

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu walitambua familia zilizoathirika eneo la Rachuonyo Kaskazini ili zifadhiliwe Sh5,000 kila familia kukodisha nyumba.

Naibu Kamishna wa Rachuonyo Kaskazini, Bw James Mabeya alisema kufikia Jumamosi, zaidi ya familia 300 zilikuwa zimekosa makao katika eneo hilo baada ya kuathiriwa na mafuriko.

Familia hizo zinatoka Osodo, Kobuya, Kobala na Chuowe katika Wadi ya Wang’ Chieng’.

Bw Mabeya alisema mfumo huo mpya unalenga kuhakikisha kuwa watu hawakusanyiki eneo moja ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Kitaifa, imekadiriwa takriban watu 30,000 wamehama makwao kwa sababu ya mafuriko. Katika vijiji vya Kimbo na Juja, Kaunti ya Kiambu, familia 200 zimeachwa na mahangaiko baada ya mvua kubwa kuharibu nyumba zao.

Wakazi hao walisema usiku wa kuamkia Jumamosi walipata mafuriko mkubwa ndani ya nyumba zao.

Mmoja wa wakazi, Bi Jane Njeri alisema amepoteza mali yake yote.

Kwingineko, Mamia ya wenyeji katika Kaunti-ndogo ya Mogotio, Kaunti ya Baringo wamepoteza makazi baada ya maporomoko ya ardhi kufuatia mvua kubwa kunyesha katika eneo hilo.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika ni vijiji vya Sirwa, Kaplaimoi, Sore, Kapurkei, Chepkoiyo na Makrip ambapo wenyeji wamelazimika kukimbilia nyanda za juu.

Zaidi ya watu 700 waliohamishwa sasa wamelazimika kupiga kambi katika Shule za Msingi za Kaplaimoi na Sore hadi mvua itakapopungua.

Barabara zinazounganisha Kipng’rom, Sirwa, Sore, Kaplaimoi, Kapurkei, Kiptuno na Makirip pia zimekatika kabisa kufuatia mvua kubwa.

Kulingana na wenyeji, zaidi ya watu 19,000 wanaopakana na Ziwa Baringo pia wako katika hatari ya kuhamishwa ikiwa mvua kubwa itaendelea kunyesha mwezi ujao. Walitaja maeneo yaliyo karibu na ziwa kama Ruggus, Kiserian, Sokotei, Ng’ambo, Salabani, Meisori, Kampi Samaki, Loruk, Katuit na Komolion kama yaliyo hatarini.

Vijiji vingine ambavyo viko hatarini katika mafuriko ya Baringo Kusini ni pamoja na Kokwo, Ng’ambo, Sintaan, Loropil, Salabani, Leswo, Longewan, Ildepe-Osinya, Eldume na maeneo ya Ilng’arua.

 

Ripoti za George Odiwuor, Lawrence Ongaro na Florah Koech