Habari za Kaunti

Waathiriwa wa mafuriko wataabika baada ya kambi kufungwa

January 5th, 2024 3 min read

NA LUCY MKANYIKA

FAMILIA za waliolazimika kuondoka katika maboma yao kwa sababu ya mafuriko katika eneo la Voi, Kaunti ya Taita Taveta zinakabiliwa na changamoto ya kuendeleza maisha yao baada ya serikali kufunga kambi walimokuwa wakiishi kwa wiki tatu zilizopita. 

Kambi nne zilizoanzishwa katika Shule ya Msingi ya Voi, Shule ya Msingi ya Ikanga, Shule ya Msingi ya Ndii na Kwa Mstapha, zilifungwa mnamo Ijumaa baada ya serikali kusema imekamilisha jukumu lake la kuwasitiri waathiriwa hao.

Hata hivyo, baadhi ya waathiriwa, ambao walipoteza nyumba na mali zao kutokana na mitaro na mito kujaa maji, walielezea changamoto zao kwani hawakuwa na mahali pa kuenda.

Serikali ilisema kuwa ilifunga kambi hizo kuruhusu shule kujiandaa kufunguliwa kwa kipindi cha wiki mbili zijazo.

Waathiriwa walipokea bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na unga wa mahindi, unga wa ngano, maharagwe, mafuta ya kupikia, mchele, mikeka ya kulalia, vyandarua, sabuni, dawa za meno, na mswaki ili kuwasaidia kurejelea maisha yao.

Baadhi ya waathiriwa ambao walipoteza mali yao yote katika mafuriko waliitaka serikali kuongeza muda wao kambini au kutafuta mahali pengine pa kuwahamisha.

Baadhi yao walilazimika kutafuta makao kwa wasamaria wema na majirani wakati wanapoendelea kujipanga kimaisha.

Bi Grace Mwavua ameitaka serikali na wasamaria wema kumsaidia kuanza maisha yake upya kwa kumjengea nyumba na kupata makazi bora.

Bi Mwavua alisema wanashukuru kwa msaada waliopokea kutoka kwa serikali na wafadhili wengine, lakini bado wako katika hali mbaya.

“Sina nyumba, sina kazi, sina chakula, sina nguo,” alisema mama huyo wa watoto watatu ambaye alikuwa akiishi kwenye kambi ya Ikanga.

Bi Mwavua alikuwa akiuza mboga kwenye soko la Caltex mjini Voi, lakini biashara yake iliathiriwa baada ya mafuriko kutoka kwenye mtaro kusomba nyumba yake na mali zake zote.

Alisema hana pesa za kuanzisha upya biashara yake.

“Nimelazimika kukodisha chumba hapa Ikanga kuanza upya maisha yangu lakini sijui nianzie wapi. Nimekuwa nikitegemea chakula cha msaada na nguo tulizogawiwa kambini. Sasa wameifunga, sijui nitakavyoishi na watoto wangu,” alisema.

Mwathiriwa mwingine, Bi Patience Wawuda, alisema hii ni mara ya tatu kufurushwa na mafuriko nyumbani kwake katika eneo la Shauri Moyo kando ya Mto Voi.

“Niliathiriwa mwaka wa 2007, 2019 na 2023. Kila kunaponyesha nina wasiwasi kwa sababu mto umegeuza mkondo wake,” alisema Bi Wawuda.

Alikaa kwenye kambi ya Shule ya Msingi ya Voi hadi ilipofungwa baada ya nyumba yake ya vyumba viwili kuharibiwa na mafuriko.

“Chakula tulichopewa ni ndogo kitadumu kwa siku chache tu. Ninaishi na wajukuu wangu ambao wananitegemea,” alisema.

Alisema ikiwa serikali inataka kuwahamisha mahali salama basi inapaswa kuwahakikishia wakazi kwamba ardhi hiyo ni yao.

“Tunaogopa kwamba serikali inaweza kutupa ardhi na baadaye kudai kwamba ilikuwa ni ya muda,” alisema.

Bw Joram Oranga, mratibu wa  Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya katika kaunti ya Taita-Taveta ambalo lilikuwa likisimamia kambi hizo, alisema kuwa kufungwa kwa kambi hizo kunalenga kuziwezesha familia kuendelea na maisha yao kwani mvua imepungua.

Waathiriwa wa mafuriko mjini Voi katika Kaunti ya Taita Taveta wapokea chakula kabla ya kuondolewa katika kambi mnamo Desemba 29, 2023. PICHA | LUCY MKANYIKA

“Hatutarajii mafuriko ndiposa tumewaacha waweze kujenga upya maisha yao. Pia, hatuwezi kuendelea kuendesha kambi kwani shule zinafunguliwa na tunapanga kusafisha madarasa kabla ya kufunguliwa kwa shule wiki ijayo,” alisema.

Alisema kuwa waathiriwa walipewa chakula cha kutosha cha msaada na bidhaa zingine za kudumu kwa mwezi mmoja.

“Wale ambao nyumba zao ziliharibiwa kabisa na mafuriko watalazimika kuishi na jamaa au majirani. Kamati itatoa mwelekeo,” alisema.

Jumla ya familia 232, ziliathirika na kusitiriwa kwenye kambi hizo.

Afisa Mkuu wa mipango maalum katika kaunti hiyo, Bw Harrison Mkala, alisema walitambua familia 19 ambazo hazikuwa na mahali pa kwenda baada ya nyumba zao kuharibiwa kabisa na mafuriko.

Alisema familia hizo zitapewa makao kwa kambi ya Mstapha kwa miezi mitatu hadi watakapoweza kuendeleza maisha yao.

Aidha Waziri wa Ardhi wa kaunti hiyo Bi Elizabeth Mkongo, alisema tayari wameanza mchakato wa kutafuta ardhi mbadala ya kuwahamisha wanaoishi kando ya Mto Voi ili kuzuia maafa zaidi.