Habari MsetoMakala

Waathiriwa wa uvamizi wateseka kimya vijijini

February 19th, 2018 3 min read

Na BONIFACE MWANIKI

Kwa ufupi:

  • Mateso aliyopitia  mikononi mwa Al shabaab na majeraha yamesababisha mabadiliko makubwa maishani mwake
  • Aliona damu ikitapakaa kila mahali na marafiki zake wakiguna kwa uchungu. Yeye alirushwa mbali na mlipuko uliotokea
  • Amepitia maumivu mengi tangu shambulio hilo na sasa anahitajika takribani Sh200,000 ili kufanyiwa upasuaji
  • Serikali inafaa kuwapa msaada waathiriwa wa mashambulio ya kigaidi kwani familia hizi hupitia masaibu mengi

WAATHIRIWA wa shambulio la kigaidi katika Kanisa la AIC mjini Garissa mnamo 2012, wamesimulia kwa mara ya kwanza masaibu waliyopitia waliposhambuliwa na magaidi wa Al Shabaab.

Bi Gladys Munyambu, kutoka eneo la Musuani, eneo la Mwingi katika Kaunti ya Kitui asema walishambuliwa wakiwa wanaendelea na maombi katika kanisa.

“Tulisikia milipuko mikubwa kanisani mahubiri yalipokuwa yakiendelea. Hadi leo siamini niliyoyaona siku hiyo mwaka wa 2012,” aeleza Bi Munyambu.

BI Gladys Munyambu akionyesha jeraha alilopata kwenye shambulio katika kanisa la AIC Garissa mnamo 2012. Picha/ Maktaba

Akiwa mmoja wa walionusurika kifo baada ya shambulio la kigaidi la Julai 1, 2012, anasema katu hatasahau mateso aliyopitia siku hiyo mikononi mwa magaidi wa Al shabaab na majeraha aliyopata siku hiyo ambayo yamesababisha mabadiliko makubwa maishani mwake.

“Niliamka kama kawaida na kuenda kanisani pamoja na familia yangu. Tuliendelea vizuri na mahubiri hadi mwendo wa saa nne. Ghafla tulisikia mlipuko mkubwa.

Mwanzo tulipuuza tukidhani ni mawe yaliyotupwa kwenye mabati lakini baadaye tukagundua kwamba halikuwa jambo la kawaida. Wanaume wawili waliingia kanisani wakiwa wamejifunika nyuso na wakaanza kufyatua marisasi kila upande. Hapo ndipo tulipojua kuwa maisha yetu yalikuwa hatarini,” alisimulia Bi Gladys.

 

Damu

Mwanamke huyu anaeleza kuwa aliona damu ikitapakaa kila mahali na marafiki zake wakiguna kwa uchungu. Yeye alirushwa mbali na mlipuko uliotokea karibu naye na akapoteza fahamu.

Bi Peninah Kituku ambaye pia alijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi katika kanisa la AIC Garissa. Picha/Boniface Mwaniki

“Niliamshwa na kelele za watoto wangu wakiita ‘mama’, ‘mama’ amka, nikiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali kuu ya Garissa. Nilimuona pia mume wangu kando yangu na hapo nikajua kuwa familia yangu iliponea shambulio hilo,” aliongeza Bi Munyambu.

Wakati wa shambulio hilo, watu 14 waliuawa. Wakati huo Kenya ilishuhudia mashambulio mengi ya kigaidi. Mashambulio makanisani yalionekana kama jaribio la Al Shabaab kuleta uadui baina ya Wakristo na Waislamu.

Yeye alipigwa risasi kwenye mguu wa kulia na vidole vyote vikakatika.

“Nililazwa katika hospitali ya Garissa kwa muda wa miezi mitatu kisha nikahamishiwa hospitali ya Kijabe. Tangu siku hiyo nimefanyiwa upasuaji mara 11 na bado sijamaliza matibabu,” akasema.  Anasema ameuza kila kitu kugharimia matibabu.

Peninnah Muli Kituku, mama wa watoto wawili, kwa upande wake asema ni kama kulikuwa na mzozo baina ya Wakristo na Waislamu kabla ya shambulio hilo.

“Nilipata fahamu na kujipata kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Garissa pamoja na waumini wengine wengi.

Mguu wangu wa kushoto ulikuwa na jeraha kubwa sana na tangu siku hiyo nimekuwa nikienda kliniki mjini Garissa ili kupokea matibabu zaidi,” alisimulia Bi Kituku.

 

Maumivu

Bi Kituku anaeleza kuwa amepitia maumivu mengi tangu shambulio hilo na sasa anahitajika takribani Sh200,000 ili kufanyiwa upasuaji.

“Huwa ninapitia maumivu makubwa nikikumbuka vile biashara yangu mjini Garissa ilivyokuwa imenawiri, na sasa siwezi hata kujilipia matibabu yangu wala kulipa karo ya watoto wangu wawili walio kwenye kidato cha tatu na nne. Mguu wangu wa kushoto pia huganda mara kwa mara na hivyo siwezi kufanya kazi ya sulubu,” akasema Bi Kituku.

Bi Peninah Kituku ambaye pia alijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi katika kanisa la AIC Garissa. Picha/Boniface Mwaniki

Katika kijiji cha Wikitoo, kata ndogo ya Musuani, eneobunge la Mwingi magharibi pia yupo Naomi Joel ambaye alipoteza baba yake katika shambulio hilo. Kwa familia hiyo, kumbukumbu yao imekuwa tu kaburi la baba yao.

“Wakati wa kifo cha baba yetu nilikuwa katika darasa la nane. Mamangu amepitia wakati mgumu kunitafutia karo ili kuniwezesha kukamilisha masomo ya kidato cha nne. Serikali inafaa kuwapa msaada waathiriwa wa mashambulio ya kigaidi kwani familia hizi hupitia masaibu mengi,” akasema.

Kwa waathiriwa wa mashambulio ya kigaidi nchini, imebakia tu maombi na matumaini kuwa siku moja serikali itasikia kilio chao na kuwapa fidia ama kugharimia malipo ya gharama za matibabu.