Habari Mseto

Waathiriwa wanaohamasisha jamii kuhusu vitiligo

March 18th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

MAISHA ya Elizabeth Wangui Njee yalikuwa kawaida tangu akiwa mtoto hadi alipotimiza umri wa miaka 14 akisoma katika Shule ya Upili ya Pangani Girls.

Wakati huo alipata doa chini ya macho yake na kudhania ilikuwa chokaa lakini ilichukua muda bila kutoweka hali iliyomfanya atafute matatibu. Baadaye iligunduliwa ilikuwa vitiligo ambapo tayari viraka vilikuwa vimesambaa karibu mwili wote.

Ndivyo hali ilivyokuwa kwa mwenzake Julie Nasuju aligunduliwa kuvamiwa na vitiligo akiwa na umri wa miaka 15. Elizabeth Wangui Njee ndiye mwasisi wa Muungano wa Vitiligo Afrika Mashariki na Muungano wa mabalozi wa vitiligo Kenya.

Naye Julie Nasuju akiwa meneja wa muungano huo pia mwenyekiti wa Royal Patches pia mtangazaji wa redio mpya nchini ya mtandaoni ya ‘Need radio’.

”Hakika huwa vigumu kujikubali muda tu unapogunduliwa kuwa mwathiriwa wa vitiligo maana rangiu ya mwili huwa imebadilika,” Julie alisema na kuongeza kwamba vilitigo haina tiba.

JULIE Nasuju (kushoto) na mwenzake Elizabeth Wangui Njee walipofika katika ofisi za Taifa Leo Dijitali. Picha/ John Kimwere

Vitiligo husababishwa na kukosa seli za kuweka rangi asili mwilini. Anadokeza kuwa mwathiriwa hupitia kipindi kigumu katika jamii kabla kufahamu vitiligo hasa ni nini. Anasema wengi wakiwamo rafiki huanza kukwepa wakihofia kuambukizwa vitiligo.

Bali na viraka kusambaa mwilini huwa siyo nyepesi kama ilivyo kasumba ya wengi wasiyofahamu kuhusu vitiligo. Kwa kutofahamu vitiligo haina tiba wengi hugharamika fedha nyingi wakisaka matibabu hospitalini.

Wawili hawa ni mabalozi wa vitiligo nchini ambapo hutembea waathiriwa katika sehemu tofauti kuhamasisha jamii kuhusu hali hiyo.

Pia hutumia mitandao ya kijamii ikiwamo Facebook (vitiligo is beautifull), Instagram(vitiligo_ambassador_ea), Twitter (vitiligoambass1) pia vyombo vya habari kueneza habari kuhusu vitiligo.

”Tumetembea sehemu tofauti nchini kuhamasisha jamii kuhusu vitiligo pia kutangamana na waathiriwa kuwasambazia kofia na mafuta ya kujipaka kuzuia makali ya jua,” Julie alieleza na kuongeza kuwa kama balozi wa vitiligo wamezuru zaidi ya kaunti 40 nchini kuhamasisha jamii kuhusu tatizo hilo na kukutana na zaidi ya waathiriwa 3500.

Kulingana na utafiti asilimia mbili ya watu wote duniani ni waathiriwa wa vitiligo. Picha/ John Kimwere

Elizabeth Wangui Njee alisema ”Hapa nchini waathiriwa wengi tayari wamejikubali na kuamua kuendeleza maisha yao kama kawaida.”

Katika ziara hizo mabalozi hawa hushirikiana na bodi ya watu wenye ulemavu bila kusahau wizara ya afya.

Vitiligo ndiyo iliyochangia Wangui Njee kuteliwa mwakilishi wa wadi katika kaunti ya Nyeri muhula uliyopita ili kuwakilisha watu wenye ulemavu.

Julie Nasuju akizungumza na Taifa Leo Dijitali alisema kila mwaka husherekea siku ya vitiligo duniani hafla ambayo hufanyika mwezi Juni 25 kila mwaka ambapo mwaka inatarajiwa kuvutia wanachama wengi kinyume na kipindi kilichopita.

UTAFITI

Vitiligo hauna mpaka hushika mtu yoyote watoto na watu wazima. Kulingana na utafiti asilimia mbili ya watu wote duniani ni waathiriwa wa vitiligo. Msukumo wa mawazo kwa mwathiriwa unaweza kufanya vitiligo kusambaa katika mwili wote.

Zaidi ya watu 240 000 hapa Kenya ni waathiriwa wa vitiligo. Waathiriwa wa vitiligo hufanya wengi kubaguliwa pia huwa vigumu kupata wapenzi kwa kuhofia kuambukizwa.

Kadhalika vitiligo hufanya waathiriwa hasa wanawake na wanaume kukosa nafasi za ajira. Hata hivyo utafiti umethibitisha kwamba kamwe mwaathiriwa wa vitiligo hawezi kuambukiza asiye mwathiriwa pia wana ndoa huzaa watoto wenye rangi asili.