Nassir na Shahbal wabishania ‘Baba’

Nassir na Shahbal wabishania ‘Baba’

Na VALENTINE OBARA

WANASIASA wanaopanga kushindania tikiti ya Chama cha ODM kuwania ugavana Kaunti ya Mombasa, wameanza kutetea uaminifu wao kwa kiongozi wa chama, Bw Raila Odinga, baada ya kubainika huenda kusiwe na kura ya mchujo.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa ODM katika kaunti hiyo, Bw Mohamed Khamis, alisema mazungumzo yanaendelea chamani ili Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, wakubaliane mmoja wao ndiye awanie ugavana.

Kufikia sasa, wawili hao ndio wameonyesha ushindani mkali kutafuta tikiti hiyo ambayo pia inamezewa mate na Naibu Gavana William Kingi.

Kulingana na maafisa wa ODM, tikiti ya kuwania wadhifa wowote wa kisiasa huweza kupeanwa kwa mgombeaji mmoja bila kutumia kura ya mchujo ikiwa kuna thibitisho kwamba ana nafasi bora ya kushinda, na hilo huzingatia pia uaminifu wake kwa kanuni na malengo ya chama.

Bw Shahbal ambaye hii itakuwa ni mara yake ya tatu kuwania ugavana Mombasa, alipuuzilia mbali viongozi wanaotilia shaka uaminifu wake kwa ODM.

Mfanyabiashara huyo aliwania ugavana kupitia Chama cha Wiper mwaka wa 2013 alipohama ODM, akatumia Jubilee mwaka wa 2017 lakini akarudi ODM mapema mwaka huu 2021.

Akizungumza katika mojawapo ya mikutano yake ya kisiasa wikendi, Bw Shahbal alisema wale wanaotilia shaka uaminifu wake kwa ODM kwa msingi wa jinsi alivyobadilisha vyama katika miaka iliyopita ni wanafiki.

Kulingana naye, mienendo yake si tofauti na ile ya Bw Odinga ambaye pia amebadilisha vyama mara kadhaa tangu alipowania urais mara ya kwanza mwaka wa 1997 kupitia NDP.

Alieleza kuwa alipowania ugavana 2013, hakuwa ameiva kisiasa na katika mwaka wa 2017, anaamini alipoteza nafasi hiyo kwa vile chama alichotumia hakikuwa na ufuasi mkubwa Mombasa.

“Rafiki yangu Abdulswamad asisimame kuniambia yeye ni mwaminifu kunishinda. Mimi najuana na Raila kuanzia mwaka wa 1999. Katika mwaka wa 2000 nilisafiri naye dunia nzima tukitafuta uwekezaji Mashariki ya Kati, na 2011 tukaenda Iran pamoja kutafuta wawekezaji. Mwaka wa 2014 akanialika baada ya uchaguzi twende naye Sudan Kusini kwa sherehe za siku za uhuru katika nchi hiyo. Usiniletee mambo ya uaminifu leo, wakati watu wa Mombasa wanataka kazi, wanataka elimu, maji, usalama, na mtu atakayeunganisha watu,” akasema.

Bw Nassir ambaye azimio lake limeungwa mkono na wabunge wengi wa ODM eneo la Pwani, hutilia shaka uaminifu wa Bw Shahbal kwa chama hicho akitaja jinsi mfanyabiashara huyo alivyohamahama kutoka chama kimoja hadi kingine tangu uchaguzi wa 2013.

Wandani wake wanaojumuisha wabunge na maseneta wa Pwani humpigia debe wakisema yeye ndiye ameonyesha uaminifu zaidi kwa ODM wakati wote alipokuwa mbunge na amethibitisha kufuata misimamo ya chama bila kutikiswa.

Akizungumza wikendi, Bw Nassir alitaka mpinzani wake aeleze alikuwa wapi wakati chama hicho kilipokuwa kikihangaishwa ndani na nje ya bunge na viongozi wa serikali hasa kati ya mwaka wa 2013 hadi 2018.

“Tulipigwa vitoa machozi tukimtetea Bw Raila Odinga. Tulikimbizwa na polisi. Bungeni tumesimama kidete lakini wengine walikuwa wakichukua leseni za kandarasi wakati huo,” akadai, akiashiria kulenga jinsi Bw Shahbal alivyopokea zabuni za ujenzi kupitia kwa kampuni yake kutoka kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa.

Wawili hao pia wanajitahidi kujinadi kama wanasiasa wasiosukumwa na watu wanaotaka kuwatumia kwa manufaa ya kibinafsi, kila mmoja akidai kulenga kuwatumikia wananchi pekee.

You can share this post!

Mhariri wa zamani wa habari katika NMG afariki

WARUI: Kufeli kwa wauguzi kunaibua maswali kuhusu mfumo wa...

T L