Habari Mseto

Waboni waitaka serikali iwajengee shule ya bweni

April 8th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

JAMII ya Waboni sasa inaitaka serikali kubuni shule moja ya bweni itakayohudumia zaidi ya wanafunzi 400 kutoka vijiji vyote vya wadi ya Basuba, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Kwa zaidi ya miaka mine sasa, wanafunzi wa Wadi ya Basuba, ambao wote ni kutoka jamii ya walio wachache ya Waboni hawajakuwa wakisoma ipasavyo kutokana na hali duni ya usalama eneo hilo inayochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Licha ya serikali kufanya juhudi na kupeleka walimu eneo hilo, hali ya masomo haijaweza kuendelea kama ilivyotarajiwa huku shule zote tano za msingi, ikiwemo Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe zikihudumia wanafunzi wa chekechea (ECDE) pekee.

Wakizungumza na wanahabari mwishoni mwa juma, Mwakilishi wa Wadi ya  Basuba, Bw Deko Barissa na wazee wa jamii hiyo walisema ni changamoto kwa wanafunzi kutoka jamii ya Waboni kuendeleza masomo yao, ikizingatiwa kuwa eneo lao limekuwa likikabiliwa na changamoto za usalama zinazochangiwa na Al-Shabaab.

Mwakilishi wa Wadi ya Basuba, Bw Deko Barissa wakati wa mahojiano na Taifa Leo. Picha/ Kalume Kazungu

Waliitaka serikali kuanzisha shule ya bweni eneo la Kiangwe ili kuhudumia wanafunzi wa vijiji vitano vya Basuba.

Kadhalika waliitaka serikali kubuni kambi ya polisi au jeshi karibu na kituo hicho cha elimu ili kukiwezesha kuendelea kuhudumia wanafunzi eneo hilo na kuzuia kituo hicho kufungwa kama inavyoshuhudia kwa shule tano za Basuba.

“Ni dhahiri kwamba serikali imeshindwa kabisa kudhibiti usalama Basuba. Shule zetu hazifanyi kazi. Wanafunzi wengi bado wako majumbani. Walimu wenyewe walioajiriwa  na Tume ya Kuajiri walimu (TSC) hakuna.

Ombi letu kwa serikali ni kwamba ibuni kituo kimoja pekee cha elimu katika eneo la Kiangwe ili kuhifadhi wanafunzi wote kutoka Wadi ya Basuba. Ulinzi wa kutosha uwekwe ili wanafunzi wetu pia wasome kama wenzao kutoka maeneo mengine ya Kenya,” akasema Bw Deko.

Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet wakati alipotembelea jamii ya Waboni wanaoishi eneo la Basuba, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki. Picha/ Kalume Kazungu

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa jamii ya Waboni, Ali Gubo, alisema anaamini ikiwa kituo hicho kimoja cha elimu kitabuniwa kitasaidia kutatua tatizo la walimu kudinda kuhudumu eneo la Basuba.

Alisema eneo la Kiangwe litakuwa rahisi kufikiwa hasa kwa kupitia usafiri wa boti baharini ikilinganishwa na wakati huu ambapo usafiri wa barabarani ni changamoto.

Kwa mara kadhaa,maafisa wa usalama na raia wamepoteza maisha wakati wanapotumia barabara kuu ya Hindi kuelekea Basuba na Kiunga kutokana na hulka ya Al-Shabaab ya kutega magari barabarani na kuyalipua kwa mabomu ya ardhini.

“Ikiwa kituo cha elimu kitabuniwa Kiangwe itakuwa rahisi kwa walimu kukubali kuhudumu huko.Eneo lenyewe ni salama ikilinganishwa na sehemu zingine za Basuba. Serikali ibuni kituo hicho ili watoto wetu wasome kwa dhati,” akasema Bw Gubo.

Bi Khadija Gurba pia aliitaka serikali kuanzisha mpango wa lishe shuleni kwa wanafunzi wa Basuba hasa iwapo ombi la kujengwa kwa kituo kimoja cha elimu litakubalika.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa jamii ya Waboni, Ali Gubo wakati wa mahojiano na Taifa Leo. Picha/ Kalume Kazungu

Alisema watoto wengi eneo hilo hutoka kwa familia zisizojiweza. Jamii ya Waboni hutegemea msitu, ambapo huwinda wanyama, kuvuna asali na kuchuma matunda ya mwituni kama kitega uchumi chao.

Aidha tangu serikali ilipoanzisha operesheni ya Linda Boni ili kuwafurusha Al-Shabaab wanaoaminika kujificha msituni, jamii ya Waboni imekatazwa kuendeleza shughuli ndani yam situ wao.

Bi Gura alisema mpango wa lishe shuleni utawezesha wanafunzi kubakia shuleni kusoma na pia kuongeza idadi ya mahudhurio darasani.

“Sisi hutegemea uwindaji wanyama pori,uchumaji matunda ya mwituni na uvunaji asali.Serikali bado imetufungia nje ya msitu wetu wa Boni.Watoto wetu hawana chakula. Ikiwa serikali iko na nia njema kwa Waboni,basi ianzishe mpango wa lishe shuleni kwa wanafunzi wetu.

Watoto wetu kwa sasa hawawezi kubaki darasani kumsikiza Mwalimu akiwafundisha wakati njaa inawasumbua tumboni,” akasema Bi Gurba.