Wabunge 10 waitwa na NCIC kuhusu fujo

Wabunge 10 waitwa na NCIC kuhusu fujo

Na SAMMY WAWERU

TUME ya Uwiano na Utangamano (NCIC), imekashifu vikali fujo na vurugu zilizozuka wakati wa chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na eneo la London – Nakuru.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Dkt Samuel Kobia, alisema Jumamosi matukio yaliyoshuhudiwa ni ishara ya viungo vinavyoweza kuchochea ghasia katika uchaguzi mkuu ujao, 2022.

Afisa huyo hata hivyo alisema NCIC haitastahimili wla kuruhusu taifa kuchukua mwelekeo huo.

“Kuna dalili ambazo hatutastahimili. Kama tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa tunataka kuhakikisha kutakuwa na amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi 2022,” Askofu Kobia akasema kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Akishtumu fujo zilizotokea wakati wa chaguzi ndogo maeneobunge ya Matungu – Kaunti ya Kakamega, Kabuchai – Bungoma na wadi ya London, Nakuru, Dkt Kobia alionya kuwa viongozi na wanasiasa waliohusika watachukuliwa hatua kisheria endapo watapatikana na hatia.

Wabunge kadha walitiwa nguvuni na kufikishwa kortini, kwa tuhuma za kuhusika kuzua vurugu na pia kudaiwa kupatikana na silaha butu kwenye magari yao.

Wanajumuisha Didmus Barasa (Kimilili), Wilson Kogo (Chesumei), Nelson Koech Belgut) na seneta wa Nandi Samson Cherargei.

Wanne hao hata hivyo waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50, 000 kila mmoja.

“Kwa wale ambao hawakukamatwa, tumewatambua na tumewaamuru wafike mbele ya NCIC,” Dkt Kobia akasema.

Wabunge Gladys Wanga (Homa Bay), Feisal Bader (Msambweni), John Walukhe (Sirisia), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Fred Kapondi (Mt Elgon), Charles Were (Kasipul), Aisha Jumwa (Malindi), Chris Wamalwa (Kiminini), Cleophas Malala (seneta wa Kakamega) na Millicent Omanga (aliyekuwa seneta maalum wa Jubilee), wametakiwa kufika mbele ya tume hiyo.

You can share this post!

Nzoia, Bandari Zagawana Pointi Kwenye Mechi ya Ligi Kuu

Kenya Cup: KCB yalemea Quins kwa jasho Kabras iking’aria...