Habari

Wabunge 11 wahojiwa kwa kuzuru Somalia kisiri

March 2nd, 2020 2 min read

LEONARD ONYANGO na AMINA WAKO

WABUNGE 11 kutoka eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya, Jumapili walinaswa na polisi mara tu baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi kutoka Somalia.

Wabunge hao walielekea nchini Somalia bila idhini kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni wala Spika wa Bunge Justin Muturi inavyohitajika kisheria, kulingana na duru za Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI).

Kwa msingi huo, safari yao iliibua maswali miongoni mwa asasi za kiusalama nchini humu kuhusu nia yao kwa kiwango cha serikali kuhusisha kitengo cha kupambana na ugaidi kuwanasa walipowasili.

Walikuwa wameelekea Mogadishu Jumamosi na ripoti zinadai walikutana na maafisa wa ngazi ya juu wa idara ya usalama nchini Somalia, madai ambayo yamewafanya maafisa wa upelelezi wa humu nchini kutaka kujua kile walichoenda huko kujadili.

Wabunge hao ni Adan Ali sheikh (Mandera Kusini), Mohamed Dahir (Dadaab), Ahmed Bashane (Tarbaj), Kullow Maalim (Banisa), Ahmed Kolosh (Wajir Magharibi), Ibrahim Abdi (Lafey), Rashid Kassim (Wajir Mashariki), Mohamed Hire (Lagdera), Omar Maalim (Mandera Mashariki), Bashir Abdullahi (Mandera Kaskazini) na Adan Haji (Mandera Magharibi).

Sita kati yao wanatoka Kaunti ya Mandera, watatu kutoka Wajir na wawili wanatoka Garissa.

Waliabiri ndege ya Salaamair Air Express Flight WU-751 hadi mjini Mogadishu, Somalia. Hata hivyo, Katibu wa Usalama wa Ndani Moffat Kangi alisema waliachiliwa huru baada ya kuhojiwa, na hawatashtakiwa.

Maafisa wa polisi Jumapili walikuwa wamekita kambi katika JKIA na uwanja wa ndege wa Wilson tangu asubuhi wakiwangoja kuwanasa wabunge hao.

Usalama uliimarishwa huku polisi wakipiga doria kila lango kuhakikisha kuwa wabunge hao hawatoroki.

Magari ya Polisi wa Kupambana na Ugaidi Jumapili yalionekana yakizunguka kati ya uwanja wa JKIA na Wilson.

Kamanda wa Polisi wa Kituo cha JKIA Titus Ndungu alisema waliimarisha doria katika viwanja vya JKIA na Wilson kwa sababu hawakuwa na taarifa kuhusu ndege ambayo wabunge hao wangetumia kurejea humu nchini.

Walipowasili Kenya, maafisa wa uchunguzi walitaka kujua lengo lao kusafiri katika nchi ya kigeni bila idhini ya serikali ya Kenya.

Ripoti zinadai serikali ya Somalia inawatumia kushawishi Kenya kukoma kuunga mkono viongozi wa Jubaland – ‘nchi’ ambayo haitambuliwi na Umoja wa Mataifa – wakiongozwa na Ahmed Mohamed Islam Madobe.