HabariSiasa

Wabunge kujiongeza mshahara tena

November 19th, 2018 2 min read

Na DAVID MWERE

WABUNGE wanapanga kujiongeza tena mshahara pamoja na marupurupu mengine, miezi saba tu baada ya kupandisha mishahara yao.

Imefichuka kuwa, kupitia kwa Tume ya Huduma za Bunge (PSC), wabunge na maseneta wote kwa jumla, wanapanga kupitisha sheria ambayo itaidhinisha kuongezwa marupurpu “kila kutakapotokea sababu ya kufanya hivyo.

Ripoti kutoka kwa kamati ya bunge la taifa inayosimamia masuala ya haki na sheria imependekeza kwenye mswada huo kwamba wabunge wote 416 na maspika wa mabunge hayo, wapewe nyumba rasmi au marupurupu ya makao kwa msingi wa Sheria ya Ajira.

Mapendekezo hayo yakipitishwa, viongozi wa wengi bungeni na manaibu wao, viranja wa wengi na wachache bungeni pamoja na manaibu wao pia watapokea marupurupu hayo.

PSC husimamiwa na Spika wa Bunge la Taifa, Bw Justin Muturi.

Malipo haya yatakuwa mbali na mkopo wa Sh20 milioni wa nyumba ambao kila mbunge hupewa na kukatwa riba ya asilimia tatu kwa mwaka, ambayo lazima ikamilishwe kulipwa watakapokamilisha hatamu ya miaka mitano ya uongozi.

Kwa sasa mkopo huo hutolewa tu kwa msingi wa mwongozo bungeni wala si chini ya sheria inavyohitajika.

“Ili kuwezesha wabunge kutekeleza majukumu yao ipasavyo, huduma hizi zitatolewa kwa njia na kiwango ambacho tume itaamua mara kwa mara kwa kuzingatia kiwango kinachotolewa kwa maafisa wengine wa kitaifa,” ripoti hiyo inasema.

Kamati hiyo inayosimamiwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini, Bw William Cheptumo, iliwasilisha ripoti hiyo bungeni Alhamisi mchana na imepangiwa kujadiliwa kesho mchana.

Mswada huo unalenga pia kufanya PSC kuwa tume ya kisheria ili Bunge liwe sawa na vitengo vingine vya serikali ambavyo ni afisi ya Rais na Mahakama.

Wabunge pia wanataka magari ya serikali yenye nambari za usajili za GK sawa na wawakilishi wa kaunti, na mikopo ya kununua magari mbali na Sh7 milioni wanazopewa za kununua magari na marupurupu wanayopewa ya usafiri.

Ingawa wabunge wa Kenya huorodheshwa miongoni mwa wanaopokea malipo makubwa zaidi ulimwenguni, wamekuwa wakilalamika kwamba hawapati manufaa ikilinganishwa na mawaziri na majaji.

Licha ya haya yote, ubora wa mijadala katika mabunge hayo mawili umekuwa duni tangu mwaka uliopita baada ya Uchaguzi Mkuu.

Ripoti hiyo imependekeza pia wabunge na maseneta waongezewe malipo ya bima ya matibabu, bima ambayo itatoa huduma pia kwa jamaa zao wa mbali na wapenzi wa kando, mbali na marupurupu zaidi ya usafiri nchini na ng’ambo.

Marupurupu kwa wanaosafiri nje ya nchi hutolewa kwa kuzingatia nchi ambayo mbunge hutembelea.

Kwa sasa mwongozo uliotolewa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) inahitaji bima ya maafisa wa kitaifa itoe huduma tu kwa mke au mume mmoja na watoto wanne wenye umri wa chini ya miaka 25