Wabunge kusafiri Denmark kunoa bongo kupitisha mswada wa chakula

Wabunge kusafiri Denmark kunoa bongo kupitisha mswada wa chakula

Na SAMMY WAWERU

WABUNGE wanatarajiwa kusafiriwa nchini Denmark mwezi huu wa Novemba ili kupata mafunzo ya usalama wa chakula, kabla kupitisha mswada utakaoainisha masuala ya usalama wa chakula nchini.

Mswada huo na ambao unatarajiwa kuweka mikakati kabambe ya uzalishaji wa vyakula nchini, kuanzia shambani, matunzo, mavuno na uongezaji thamani, mdahalo wake ulianza 2012. Wizara ya Kilimo na Afya, hata hivyo zimekuwa zikitofautiana kuhusu utekelezaji wa mapendekezo.

Huku maswali yakiibuka kwa nini wadauhusika haswa wanaochangia pakubwa katika uzalishaji wa chakula nchini hawatashirikishwa katika ziara ya Denmark, Ubalozi wa Kifalme wa Danish (RDE) hapa Kenya umesema wabunge watakaosafiri watateuliwa kutoka kamati ya kilimo na afya bungeni.

Wataalamu wa kiufundi vilevile watajumuika na wabunge hao. Mchango wa zaiara kuboresha mswada Kulingana na Bw Henning Høy Nygaard, Mshauri sekta ya chakula RDE, ziara hiyo itawezesha wabunge kupata mchango kuboresha mswada wa usalama wa chakula nchini.

“Hii ndiyo mara ya kwanza tunawapeleka Denmark kupata mafunzo, na ziara yenyewe inahusishwa na mswada wa usalama wa chakula,” Bw Henning akasema, akizungumza katika warsha jijini Nairobi, iliyoandaliwa na washikadau husika katika sekta ya kilimo.

Kulingana na Bw Henning Høy Nygaard, Mshauri sekta ya chakula katika Ubalozi wa Kifalme wa Danish (RDE) hapa Kenya, ziara ya wabunge Denmark inalenga kuboresha mswada wa usalama wa chakula kabla kuwasilishwa bungeni kujadiliwa na kupitishwa…Picha zote/ SAMMY WAWERU.

Afisa huyo aidha alihakikishia Kenya kwamba Denmark itashirikiana na serikali kuafikia uslama wa chakula nchini. Denmark ni kati ya mataifa tajika ulimwenguni yaliyopiga hatua mbele katika sekta ya kilimo na ufugaji, na pia katika uongezaji wa mazao thamani, na kuzingatia usalama wa chakula.

Mazao hatari

Wadau wengi katika sekta ya kilimo wamekuwa wakizingatia uzalishaji wa chakula na kuwepo na cha kutosha, baadhi wakionekana kupuuza usalama jinsi kilimo kinavyoendeshwa.

Matumizi ya pembejeo zenye kemikali, hususan fatalaiza na dawa kukabili wadudu na magonjwa, yametajwa kuchangia kuwepo kwa mazao hatari na yanayosababisha magonjwa yanayohusishwa na lishe, kama vile Saratani.

Saratani, pia Kansa ni janga la kimataifa na ambalo limesababisha vifo vya watu wengi, ikizingatiwa kuwa ni maradhi yasiyo na tiba na ghali kuzima makali yake. Kulingana na Bw Henning, kuna haja kubwa Kenya kutathmini mikakati ya usalama wa chakula.

Kebs yakosolewa

Akikosoa jinsi Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) hukagua bidhaa madukani na kuondoa ambazo hazijaafikia ubora faafu, alisema usalama na hadhi unapaswa kuanza wakati wa upanzi wa mimea, utunzaji na uboreshaji wa mazao shambani na yanavyoongezwa thamani.

“Sote tunategemea sekta ya kilimo na ufugaji, na mazao yanapaswa kuwa salama,” Bw Henning akasisitiza. Mswada wa usalama wa chakula upo katika hatua za mwisho, kabla kujadiliwa bungeni, kulingana na Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya.

Pendekezo la shirika maalum kuhusu usalama wa chakula Waziri Munya anapendekeza kubuniwa kwa shirika maalum litakalokuwa likiangazia usalama wa mazao na chakula nchini.

“Tukiwa na shirika litakaloangazia masuala ya usalama wa chakula, kuanzia uzalishaji wa mazao shambani, mavuno hadi usindikaji, mlo unaofika mezani utakuwa salama,” Munya akaambia Taifa Leo Julai 2021, Kilimo House Jijini Nairobi.

Alisema hatua itasaidia kufuatilia uzalishaji wa chakula, kuanzia shambani, matunzo ya mazao, mavuno na kuweka mikakati bora kuyaongeza thamani.

 

You can share this post!

Mbunge apendekeza kutathminiwa kwa sheria za uchaguzi...

AKILIMALI: Jinsi bidhaa za sodo zinazoweza kudumu hadi...

T L