Habari MsetoSiasa

Wabunge Mlima Kenya wasifu rais kumpa Matiang’i mamlaka

January 28th, 2019 2 min read

GRACE GITAU na GEORGE MUNENE

WABUNGE kutoka eneo la Mlima Kenya wameonya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika uamuzi wa Rais Uhuru Kenyatta kufanya mabadiliko serikalini, wakasisitiza mabadiliko hayo hayahusu siasa za urithi wa 2022.

Wiki iliyopita, Rais Kenyatta alifanya mabadiliko serikalini akamfanya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kusimamia kamati ya mawaziri wote na kuwa mkaguzi wa utekelezaji wa miradi ya serikali.

Baadhi ya wanasiasa wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto walichukulia hatua hii kama ya kumtenga na kuvuruga juhudi zake za kumrithi Rais Kenyatta.

Lakini wabunge kadhaa wa eneo la kati wakiongozwa na Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua walisema rais ana mamlaka ya kufanya mabadiliko serikalini akitaka kuhakikisha utekelezaji wa ajenda nne kuu unatimizwa ipasavyo.

Aliungwa mkono na mwenzake wa Kangema, Bw Muturi Kigano na Mbunge wa Nyeri, Bw Ngunjiri Wambugu.

Bw Gachagua alisema ukosefu wa uratibu katika serikali kuu umesababisha miradi kukwama, mingine baada ya kuanzishwa.

“Kwa muda mrefu tumeshuhudia ukosefu wa uratibu bora katika maendeleo lakini kupitia kwa kamati hii, rais anaweza kufuatilia kwa karibu miradi yote,” akasema.

Mbunge huyo ambaye wakati mwingi amekuwa akimhakikishia Bw Ruto kwamba ataungwa mkono kwa urais na jamii za Mlima Kenya, alikosoa viongozi ambao “wana mitazamo mingi ya kisiasa katika kila hatua inayochukuliwa na rais”.

Aliongeza: “Mbona baadhi ya wanasiasa wanalalamika zaidi ya wengine? Kama naibu rais aliridhishwa na agizo hilo kuu la rais na halalamiki, mbona wengine wana wasiwasi?”

Alisema tayari ameitisha mkutano na maafisa wa serikali kuu wanaohudumu katika eneobunge lake ili kujadiliana kuhusu hali ya miradi inayoendelezwa na wizara mbalimbali.

Kulingana na Bw Kigano, amri ya rais itasaidia kufanya mawaziri wavivu wawajibike zaidi katika majukumu yao ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaharakishwa kwa sababu rais atakuwa anapokea ripoti mara kwa mara kuhusu kila mradi.

“Tuna baadhi ya wanasiasa ambao lazima wasukumwe lakini hili litabadilika. Rais anafaa kupewa nafasi ya kuendesha serikali kwa njia anayoona itamsaidia kuacha sifa bora nchini,” akasema.

Mbunge wa Imenti Kusini, Bw kathuri Murungi alisema hakuna nia yoyote mbaya katika kubadilisha majukumu serikalini kwani rais ana lengo la kuacha sifa nzuri atakapokamilisha hatamu yake ya pili iliyo ya mwisho ya uongozi wa taifa.

“Waziri matiang’i amepewa jukumu la kuongoza kikosi hicho kwa sababu ya utendakazi wake katika wizara za Elimu na ya Usalama wa Ndani. Waziri wa Fedha ni naibu mwenyekiti ili atoe ushauri wake kuhusu uwepo wa rasilimali. Hakuna siasa hapo kwa mtazamo wangu,” akasema Bw Kathuri.