Habari Mseto

Wabunge Pwani wakosoa sheria inayotoa fursa bandari kubinafsishwa

July 4th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

WABUNGE kutoka eneo la Pwani, Jumatano walieleza kutofurahishwa kwao na mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu mswada wa usimamizi wa Bandari, baada yake kupendekeza kwamba hata shirika la kibinafsi linaweza kuendesha bandari.

Katika mswada huo ambao ulifanywa sheria Jumanne, shirika la kibinafsi linaweza kuendesha bandari, bora serikali iwe inadhibiti sekta hiyo, ama serikali yenyewe iiendeshe.

Wabunge wapatao 13, hata hivyo, walijitokeza kueleza ghadhabu zao baada ya kushindwa kuuangusha mswada bungeni Jumanne, wakisema kuna mpango wa kupeana Bandari ya Mombasa kwa shirika la kigeni.

Mbunge wa Mvita, Abdulswammad Nasser (kushoto) akiwa na viongozi wengine wa Pwani Julai 3, 2019, katika majengo ya bunge. Picha/ Peter Mburu

Wabunge hao, badala yake, wanataka shirika litakaloendesha bandari liwe linamilikiwa na serikali kikamilifu.

Walisema baada ya sheria hiyo mpya kupitishwa, shirika la kutoka Uitaliano litakuwa likisimamia bandari, kwani litakuwa na usimamizi wa asilimia 47, serikali ikiwa na asilimia 53.

“Tulielewana na bunge zima kuwa ikiwa mfumo wa kusimamia bandari utaundwa, iendeshwe na serikali kikamilifu. Zaidi ya asilimia 70 ya wabunge walikubaliana nasi,” akasema mbunge wa Mvita Abdulswammad Nasser.

Hisa

Hata hivyo, mbunge huyo alisema mswada huo ulipofikishwa kwa Rais, aliurejesha bungeni kwa mapendekezo kuwa bandari inaweza kumilikiwa na serikali ama idhibitiwe na serikali endapo itaendeshwa na shirika la kibinafsi.

“Sasa tunaona fursa ambapo mtu anaweza kuja na kuipa serikali hisa chache kisha kuanza kuendesha bandari. Unapopeana bandari yetu kwa miaka 33, ni kupeana rasilimali zetu kizazi kizima. Tunaheshimu katiba lakini hatukubaliani kabisa na kile kimefanyika,” akasema Bw Nasser.

Wabunge zaidi ya 13 waliokuwa wakihutubia wanahabari bungeni walishangaa ni kwanini wakati taifa linanyima shirika la Kenya Airways fursa ya kusimamia viwanja vya ndege kwa kuhofia rasilimali za umma hazitafaa taifa, kwa upande mwingine linaacha bandari kusimamiwa na shirika la kibinafsi.

Viongozi hao vilevile walisema haiwezekani kuwa serikali imetumia takriban Sh43 bilioni kuunda miundomsingi katika bandari, kisha ipokeze shirika la kibinafsi kuisimamia.

“Hili ni suala ambalo linawagusa Wakenya, si wakazi wa Pwani peke yao. Bandari ya Mombasa imekuwapo vizazi vyote,” akasema mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani.