Habari

Wabunge vijana watisha kuchochea maandamano ikiwa walimu wa BoM hawatalipwa

September 11th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Wabunge Vijana Nchini (KYPA) umetisha kuandaa maandamano kote nchini ikiwa Serikali haitakuwa imewalipa walimu walioajiriwa na bodi za shule (BoM) ifikapo Jumatatu, Septemba 14, 2020.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwenzake Naisula Lesuuda wamewaambia wanahabari Ijumaa katika majengo ya bunge kwamba watafanya mkutano siku hiyo kupanga maandamano hayo ikiwa kufikia siku hiyo walimu hao hawatakuwa wamelipwa.

“Tunajua kuwa Waziri Msaidizi wa Elimu Zack Kinuthia na Katibu katika Wizara hiyo Belio Kipsang’ walisema kuwa walimu hao watalipwa Ijumaa, Septemba 11, 2020. Kwa hivyo, tunaonya kwamba ikiwa malipo hayo hayatatolewa jinsi walivyosema, serikali ijiandae kwa maandanamo makubwa kuanzia Jumatatu,” akasema Bw Owino ambaye ni Mbunge wa Embakasi Mashariki.

“Nawataka polisi wajiandae kwa vitoa machozi kwa sababu maandamano hayo yatagatuliwa hadi katika ngazi ya wadi katika kaunti zote 47 nchini,” akasema Mbunge huyo wa ODM.

Bw Owino ni Katibu Mkuu wa KYPA, ambayo mwenyekiti wake ni Mbunge wa Langata, Nixon Korir (Jubilee).

Bi Lesuuda ambaye ni mbunge wa Samburu Magharibi alisema malipo ya walimu hao hayafai kucheleweshwa kwa sababu tayari serikali imesema kuwa imetoa Sh1.76 bilioni kugharimia.

“Walimu hawa wamelalamika kwetu sisi wabunge wanachama wa KYPA kila mara kwani wamesalia bila mishahara yoyote tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kilipotangazwa nchini mnamo Machi 13, 2020 na shule zikafungwa mnamo Machi 15, 2020,” akasema Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Kanu.

Akaongeza: “Inasikitisha kuwa zaidi ya mwezi mmoja umepita tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoamuru walimu hawa walipwe. Kwa hivyo, malipo hayo yatolewe Ijumaa jinsi Wizara ya Elimu ilivyoahidi la sivyo, tutapanga maandamano vile mwenzangu alivyosema.”

Bi Lesuuda alisema wabunge wa BoM hujaza pengo ya uhaba wa walimu nchini na hivyo wanafaa kuthamini.

“Kulingana na Tume ya Huduma za Walimu (TSC) Kenya ina uhaba wa jumla ya walimu 100,000. Ili kutoa afueni kwa uhaba huo Bodi za Shule zimeajiri zaidi ya walimu 80,000 ambao hulipwa kutoka na karo za wanafunzi. Kwa hivyo, tangu shule zilipofungwa walimu hao hawajalipwa.” akasema.

Kulingaana na Katibu Dkt Kipsang’ ni walimu 43,000 pekee kati ya orodha ya walimu 126,000 iliyowasilishwa na walimu wakuu watalipwa. Hii ni baada ya tathmini iliyoendeshwa na Wizara hiyo pamoja na Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) kuondoa wengine 83,000 ambao ilisemekana ni ghushi.

Bw Owino aliahidi kuwa hivi karibuni atawasilisha hoja bunge kuitaka serikali itenge hazina maalum ya kuwalipa walimu wa BoM.

“Hii ndio njia ya kipekee ya kuwakinga dhidi ya athari na matukio ya ghafla kama vile janga la corona,” akasema.