Wabunge wa Kenya Kwanza wadai maandamano ya Raila ni sawa na jaribio la kupindua serikali

Wabunge wa Kenya Kwanza wadai maandamano ya Raila ni sawa na jaribio la kupindua serikali

NA CHARLES WASONGA

KUNDI la wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza wamedai kuwa maandamano yaliyoitishwa Jumatatu jijini Nairobi na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ni njama ya kupindua serikali ya Rais William Ruto.

Wakiongozwa na mbunge wa Kwanza Ferdinand Wanyonyi, wabunge hao wapatao 20 hata hivyo walishikilia kuwa mipango ya kiongozi huyo wa Azimio itaambulia patupu.

“Maandamano yaliyoitishwa na Bw Odinga ni mabaya na ni mbinu iliyopitwa na wakati. Ni jaribio la kupindua serikali iliyochaguliwa kihalali,” akasema Bw Wanyonyi ambaye alichaguliwa kuingia bungeni kwa tiketi ya Ford Kenya.

Akaongeza: “Tungependa kuwaambia kwamba milango ya kuingia serikalini kupitia nyuma ilifungwa baada ya uchaguzi uliopita. Haitafunguliwa tena. Sio wakati wa utawala wa Ruto.”

Bw Wanyonyi alimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kuwalinda Wakenya na mali yao mnamo Jumatatu Machi 20, wakati ambao Azimio imetangaza kufanya maandamana jijini Nairobi kwa “lengo la kuelekea Ikulu.”

Baadhi ya wabunge aliokuwa pamoja na Bw Wanyonyi alitoa changamoto kwa Bw Odinga kuweka jamaa zake mbele wakati wa maandamano ikiwa kweli anaongozwa na nia njema.

“Tunamtaka Bw Odinga kuita mkewe, ndugu yake Oburu, bintiye Winnie na watu wengine wa familia yake waongoze maandamano badala ya kutumia watoto wa Wakenya masikini kuendeleza ajenda zake za kibinafsi,” akasema Mbunge wa Maragua Mary Wamaua.

Wabunge wengine waliokuwepo ni pamoja na; George Gitonga Murugara (Tharaka), Dancan Maina (Nyeri Mjini), George Koimburi (Juja), Peter Kihungi (Kangema), Joseph Chororet (Kipkelion Mashariki) Eric Wamumbi (Mathira) miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Mchanga wa ufuoni unavyotia ladha njugu

Wandayi awaomba waajiri kuwapa wafanyakazi ruhusa ya...

T L