Siasa

Wabunge wa Kiambu wamuandaa Alice Ng’ang’a kwa ugavana 2027

March 21st, 2024 2 min read

NA LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wanane kutoka Kaunti ya Kiambu wameungana katika kinachoonekana ni kumvumisha mbunge wa Thika Alice Ng’ang’a kumuandaa kuwania ugavana mwaka wa 2027.

Mnamo Jumatatu, viongozi hao walizuru eneo la Ngoingwa mjini Thika kupima mwitikio wa wananchi kuhusu njama yao.

Viongozi hao nyuma ya Bi Ng’ang’a ni mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe, mbunge wa Lari Mburu Kahangara, mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah, mbunge wa Juja George Koimburi, mbunge wa Kabete James ‘Wamacukuru’ Githua Kamau, seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kiambu Anne Wamuratha, na mbunge wa Kiambaa John ‘Kawanjiku’ Njuguna.

Viongozi hao walikutana wakati ambapo Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi analaumiwa kwamba anatekeleza miradi bila kuwahusisha wabunge kadhaa na viongozi wengine.

Aidha walimsifu Bi Ng’ang’a na kumuita ‘Mama Simba’ huku wakimtaja kama kiongozi wa pekee anayeweza kupambana na gavana Wamatangi.

Kulingana na viongozi hao, ni kwamba wamefanya utafiti wao na kugundua ya kwamba uongozi wa wanawake ni bora.

Walitoa mfano wa Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Gavana wa Embu Cecily Mbarire na Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti.

Kawanjiku alidai ya kwamba miradi ambayo gavana Wamatangi anajihusisha nayo zaidi mashinani ni kugawa vifaranga na nguruwe kwa wananchi, jambo alilotaja kama sio muhimu kwa mwananchi wakati huu.

Viongozi hao walimsuta Bw Wamatangi kwa kufanya kazi kibinafsi bila kuhusisha viongozi wengine.

Walisema wananchi pia huwa hawahusishwi kikamilifu katika miradi kadhaa ambayo gavana anaendesha.

“Mimi kiongozi niliye katika Seneti nimekuwa nikifuatilia utumizi mbaya wa fedha katika Kaunti ya Kiambu,” alisema Bw Wa Thangw’a.

Bi Ng’ang’a alikuwa ameandamana na viongozi hao kuzindua mradi wa kituo cha polisi cha Ngoingwa mjini Thika ambacho ujenzi wake utagharimu Sh30 milioni.

Bi Ng’ang’ a alisema wataendelea kutumikia wananchi kwa njia ifaayo. Aidha, aliahidi mradi wa soko kwa wakazi wa Makongeni.

“Wakazi wa Makongeni watapata soko la kisasa ambapo kila mmoja wa wauzaji atapewa sehemu yake,” alisema Bi Ng’ang’a.

Alisema wao kama viongozi wa Kiambu wataendelea kufanyia wananchi kazi kwa kujitolea.