Wabunge wa maeneo kame wataka NG-CDF zaidi

Wabunge wa maeneo kame wataka NG-CDF zaidi

Na SAMMY LUTTA

WABUNGE wawili kutoka Kaunti ya Turkana wamependekeza kubadilishwa kwa mfumo wa ugavi wa fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneo-bunge (NG-CDF) ili kuinua viwango vya elimu katika maeneo kame nchini (ASAL).

Mbunge wa Turkana Mashariki, Ali Lokiru na mwenzake wa Turkana ya Kati, John Lodepe walisema mfumo wa sasa ambapo kila eneo-bunge linapokea Sh137 milioni unafaa kubadilishwa ili kuongeza mgao wa maeneo kame na yenye umasikini.

Wawili hao walisema, umasikini mkubwa na utovu wa usalama katika maeneo kame nchini ndio uliochangia kudorora kwa viwango vya elimu na ukosefu wa elimu katika shule za maeneo ya ASAL.

Bw Lokiru aliwataka wenzake katika bunge la kitaifa kuunda sheria itakayowezesha kaunti masikini katika maeneo kame, kuongezewa mgao wa fedha za NG-CDF kama hatua ya kuhakikisha usawa.

“Kwa mfano, katika eneo-bunge la Turkana Mashariki tunategemea fedha za NG-CDF kujenga shule na kulipa karo za wanafunzi. Watoto wetu wakisoma ndipo wataweza kufikia ndoto zao za kuwa madaktari, walimu, marubani na wahandishi, hali ambayo itainua maisha ya familia zao,” akasema.

Kwa upande wake Bw Lodepe alilalamikia uhaba wa fedha za NG-CDF kiasi kwamba inawalazimu baadhi ya wanafunzi katika eneo-bunge lake kutegemea wahisani wengine kuwalipia karo

“Watoto wengine hutoka familia masikini ambazo huwa zimepoteza mifugo wao kutokana na ukame na mashambulio ya wezi wa mifugo. Vile vile, shule nyingi hazina vifaa, hali inayochangia matokeo duni.”

You can share this post!

Hofu wezi wakijaribu kufukua mwili wa mbunge

Musyoka akoleza urafiki wa kisiasa na Lenku